Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwahimiza vijana kufanya kazi kwa staha, weledi na uadilifu ili kuzitumia rasilimali zilizopo nchini kujiletea maendeleo.
“Nchi yetu imebarikiwa fursa nyingi za kiuchumi, ili jamii ione matunda ya uwepo wa fursa hizo tunategemea sana nguvu kazi ya vijana katika kuzitumia rasilimali zilizopo”.
Ametoa wito huo leo Jumapili (Oktoba 01, 2023) wakati wa Jubilee ya miaka 125 ya Uinjilishaji katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea, kwenye kilima cha Peramiho, Songea mkoani Ruvuma.
Aidha, amezisihi Taasisi za Dini kuweka mipango mahsusi na shirikishi ya malezi ya vijana. “Tumieni nafasi zenu kuongeza msukumo wa malezi kwa vijana kwa kuweka mifumo ya kuwafuatilia kwa karibu na kuhimiza ushiriki wao kwenye vyama vya kitume”
Kadhalika, Mhe. Majaliwa amewasihi viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa masuala ya kipaumbele yanayohusu ustawi wa Taifa.
“Niwasihi sana mtuunge mkono kuhamasisha uhifadhi wa mzingira na matumizi ya nishati safi, kampeni za kupanda miti na usafi wa mazingira, kukemea vikali vitendo vya mmomonyoko wa maadili, matumizi ya dawa za kulevya na kukemea vitendo vya rushwa”.
Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyapongeza madhehebu ya dini kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwenye sekta za elimu, afya, maji na huduma nyingine za kijamii hasa katika maeneo ya pembezoni.
“Kazi hiyo mnayoifanya ya kutoa huduma kwa jamii ni kuunga mkono dhamira ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kusogeza huduma zote muhimu karibu na wananchi”
Katika Jubilee hiyo, Rais Dkt. Samia ametoa shilingi milioni kumi kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 125 ya jubilee ya Uinjilishaji katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea.
Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa katika shughuli mbalimbali za huduma za jamii na uinjilishaji zinazofanywa na kanisa katoliki nchini.