Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ametoa rai kwa Vilabu vya Mpira wa Miguu nchini kuunga mkono juhudi za kupinga ukatili kwa Wanawake na watoto wa jinsia zote ili kukomesha na kumaliza vitendo hivyo kwenye jamii.
Mhe. Mwinjuma ametoa rai hiyo leo Oktoba 18, 2023 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa jinsia zote kupitia mchezo wa mpira wa miguu ijulikanayo kama "Piga mpira sio Mwanamke"
Amesema ni wakati muafaka kwa vijana wa kiume, wakina baba kujadili tatizo hilo ili kuwarithisha watoto Taifa lenye utulivu, amani, upendo na Maendeleo huku akibainisha kuwa kampeni hiyo ambayo iko chini ya Taasisi ya Thamani Women Tanzania ikiongozwa na Mkurugenzi wake, Nafue Nyange mpaka sasa imeungwa mkono na Vilabu vya Simba SC, Azam FC na Singida Fountain Gate.
"Mchezo wa mpira wa miguu umesaida kuunganisha watu na jamii. Jambo hili linaufanya mpira uwe zaidi ya mchezo na zana muhimu ya kuvunja vizuizi vya kijamii na kiutamaduni nje ya uwanja. Wachezaji kutoka nyanja mbalimbali wana jukumu la kufanya kazi pamoja kufikia lengo moja la ushindi dhidi ya timu pinzani. Leo tunashuhudia vilabu hivi vitatu vikiungana dhidi ya mpinzani mmoja Ukatili"- amesisitiza Mhe. Hamis Mwinjuma