Serikali imesema vikao vya kupokea na kujadili changamoto za Muungano bado vipo na vitaendelea kuwepo kutokana na umuhimu wake katika mustakabali wa Muungano wetu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Novemba 07, 2022.
Mbunge wa Mwera, Mhe. Zahor Mohammed Haji alitaka kufahamu kama vikao vya kupokea na kujadili changamoto za Muungano kama vipo na vilikaa mara ya mwisho lini.
Katika majibu ya msingi, Mhe. Khamis alisema vikao hivyo hufanyika kwa mujibu wa Mwongozo wa Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kushughulikia Masuala ya Muungano ambao umeridhiwa na pande zote mbili za Muungano.
Aidha, alisema katika Mwongozo huo kikao cha Kamati ya Pamoja hufanyika mara moja kwa mwaka, Kikao cha Mawaziri hufanyika mara moja kwa mwaka, Kikao cha Makatibu Wakuu hufanyika mara mbili kwa mwaka na Kikao cha Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja hufanyika mara nne kwa mwaka.
Mhe. Khamis aliongeza kuwa kwa mwaka 2021/22, vikao hivyo vilifanyika kwa mujibu wa Mwongozo huo ambapo kikao cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano kilifanyika Agosti 24, 2021.
Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alifafanua kuwa katika Kikao hicho hoja 11 kati ya 18 zilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.
Alisema tayari hoja mbalimbali zimeshapatiwa ufumbuzi zikiwemo Uvuvi wa Bahari Kuu, Mgawanyo wa Mapato, Mapato yanayotokana na Idara ya Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar na Ucheleweshaji wa Miradi ya Maendeleo.
”Mheshimiwa Spika katika hili kwa mfano kusainiwa kwa mikataba ya miradi ya maendeleo kule Zanzibar hili limeshapatiwa ufumbuzi ikiwemo, kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa Hospitali ya Biguni, ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, ujenzi wa Barabara Chake Macho Manne kuelekea Meli Tano kueleka kwa Binti Abeid hadi Wete tayari yote haya yameshapatiwa ufumbuzi,” alisema.