Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

“Vijana 1,218 Pugu Wachangamkia Ajira za JPM Reli ya Standard Gauge”
Jun 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Judith Mhina.

Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, la kutoa kipaumbele cha ajira kwa Vijana wa Kata ya Pugu limepokelewa vizuri ambapo takriban vijana 1218 wamehamasika na kutuma maombi ya ajira kwenye mradi wa reli ya standard gauge ulioanza kutekelezwa hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Kata za Pugu Bombani na Pugu Stesheni zenye jumla ya mitaa 8, katika mahojiano Maalum na mwandishi wa Idara ya Habari - MAELEZO.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Stesheni, Bw Sifa Makakala amesema “Pugu Stesheni ina jumla ya kaya 1,905, na wakazi 7,636 ambapo Wanawake ni 3843 na Wanaume 3793. Aidha, kati ya hao Vijana wapo 230 na idadi ya Vijana walioomba ajira  ni Wanaume 396 na Wanawake 88”.

Makakala amesema: “Vijana wengine walioomba ajira walitoka nje ya kata yetu, ambao ni kutoka Mkoa wa Dodoma (3) Iringa (3), Kagera (6), Morogoro (16), Mwanza (8), Pwani (14), Singida (7), Shinyanga (3) na Tanga (10).

Aidha, hapa Dar-Es-Salaam waliotoka nje ya kata ya Pugu Stesheni ni Makuka Mbagala (1) Kivule Majohe (2) Ulongoni B (11) Kin’gon’go kata ya Salanga, Ubungo (1) Malikasi Ukonga (3) Kichangani (15) Pugu Bombani (14) Kigogo A (13) Chanika (13).

“Mtaa wa Kinyamwezi  una kaya 4,700 ambapo kuna wakazi  7,573  ambapo Wanawake ni 4,500 na Wanaume 3,500, kati ya hao Vijana ni 2,400, waliomba ajira ni Vijana Wanaume 35 Wanawake 25”  amesema Mwenyekiti wa Mtaa huo, Bw Mkubwa David.

Mtaa wa Kwa Mustafa kuna kaya 4,100 wenye wakazi 9,705 ambapo wanawake ni 5,593 na wanaume ni 4,412 kati ya hao vijana ni 200,  walioomba kazi ni Wanawake 60 na Wanaume 214, amesema Bibi Bahati Usinzi ambaye ni mwenyekiti wa mtaa huo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Pugu Bombani, Bw Gido Lupiana amesema, “Vijana wengi wamepitisha barua zao za maombi ya ajira katika mtaa wetu, lakini kwa bahati mbaya hatukuweka kumbukumbu, kwa makisio ni zaidi ya vijana 400   ambao wameomba”.

Mtaa wa Pugu Bombani una kaya 2,928, wenye wakazi 11,815 ambapo Wanawake ni 6,518 na Wanaume 5,297 ila idadi ya vijana sijawatambua rasmi” amesema Lupiana

Akitoa ufafanuzi juu ya ajira walizoomba, Lupiana amesema ni pamoja na :  “Katibu muhtasi, madereva wa malori, katapila, magari madogo, mafundi wa kuchomea vyuma, mafundi ujenzi, wahudumu wa ofisi wahudumu wa treni, wakatishaji wa tiketi, wapishi na nguvu kazi ya usambazaji vifusi, kokoto, matofali na kazi kama hizo”.

Aliongeza kusema kuwa kata yake imepokea maombi ya mikoa mbalimbali na Wilaya nyingine za Dar-es-salaam, Pwani, Arusha, Kigoma, Singida na Mwanza.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa reli ya standard gauge, Mhandisi Maizo Madze amesema: “Maombi mengi yaliyopokelewa, kwa asilimia kubwa ni ya vijana ambao wameomba nafasi mbalimbali.

Aidha, kwa kuwa Kampuni ya ujenzi ya YAPI inahitaji watu wenye uzoefu na kazi za reli ni vyema  watumishi  wastaafu wa reli ambao bado wana nguvu kuomba nafasi za ajira za kuifundi na maombi yote yatawasilishwa kwenye ofisi ya ujenzi ya YAPI, amesema Mhandisi Madze.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli- RAHCO, Bw Masanja Kadogosi amesema: “Mradi umeelekeza ajira za kiufundi kwa raia wa Uturuki asilimia 80 na Watanzania asilimia 20. Aidha, katika asilimia 20 ya kazi za  kiufundi kampuni ya ujenzi ya YAPI inapendekeza watumishi wenye uzoefu wa mambo ya reli, pamoja na wenye uzoefu wa kazi nyingine za kiufundi kupewa kipaumbele”.

“Kuhusu ajira za kawaida yaani mtambuka na nguvu kazi  mkataba unaelekeza asilimia 80 ya waajiriwa watoke Tanzania na 20 watatoka Uturuki. Hii itatoa fursa ya pekee kwa watanzania kuajiriwa katika kazi kama madereva, katibu muhtasi, watunza store za vifaa, wahudumu, wabeba kokoto mchanga, wapishi na kazi kama hizo. Mradi wa reli ya standard gauge una jumla za nafasi za ajira 6,000 ambazo ni za watanzania”  amesisitiza Bw Kadogosi.

Bw. Kadogosi amesema: “Mpaka sasa jumla ya wafanyakazi 154 wameshaajiriwa na wanaendelea na kazi katika vituo vya maandalizi vya Soga na Ngerengere ambapo kampuni imenunua magari 9 ya kuanzia kazi”.

“Natoa wito kwa Wananchi wasiamini  watu wanaosema RAHCO imeingia nao mkataba kuwa wao ni wakala wa kutafuta wafanyakazi, ambapo tumesikia wanachukua  fedha zao na kuwadanganya kuwa watapata kazi sio kweli, na sisi tukiwakamata tutachukua hatua za kisheria, hao  ni matapeli”.  Alisisitiza Bw. Kadogosi.

Pia mtendaji Mkuu huyo  wa “RAHCO  alisema  kampuni yake haijamuajiri mtu wala kikundi wala kampuni, Wananchi mnachotakiwa kufanya ni kuleta barua ya maombi ya kazi na viambatanisho vyake na utaratibu umewekwa ili kushughulikia maombi yao kwa  uwazi bila upendeleo”.

“Tupo kwenye maandalizi ya kufungua mtandao wa RAHCO, mara utakaofunguliwa, tutaweka nafasi zote za kazi pamoja na zile za ukandarasi katika mtandao huo,pia  RAHCO  itaandaa chapisho maalum kwa  wakandarasi wazawa ili  kuwaeleza fursa zinazopatikana, waweze kuzichangamkia kama alivyosisitiza Mh.Rais,”Alisema Bw.Kadogosi.

Akiwa katika uzinduzi wa ujenzi wa reli ya standard gauge tarehe 12 Aprili Mwaka huu Rais   wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli alitoa agizo, kuwa Vijana wa Kata ya Pugu Bombani na Pugu Stesheni, wapewe upendeleo maalum katika ajira zitakazotolewa na kampuni ya ujenzi ya YAPI kutoka Uturuki.

Ni ukweli usiopingika kuwa ajira zinazotengenezwa na Rais Magufuli, zitavuka lengo na kuongezeka mara dufu na ninathubutu kusema mpaka mwaka 2020 tutashuhudia Vijana wengi wakiwa wameajiriwa au kujiajiri kwa kuwa fursa zipo nyingi mno, kutokana na kuelekea uchumi wa viwanda vya chini kati na vikubwa.

Mh. Rais Magufuli amewaandalia Vijana ajira   takriban 9,000, ambazo ni nafasi zilizoachwa wazi na watumishi wenye vyeti feki, katika juhudi huizo pia amempatia mfanyabiashara maarufu nchini Salim Said Bhakresa ekari 1,000 za kulima miwa pamoja na kujenga kiwanda cha Sukari ambacho kitaajiri zaidi ya watu 1,000 ikiwemo ajira rasmi na zisizo rasmi ambazo zitatokana na kuwepo kwa kiwanda hicho.

Pia jitihada za Mh Rais kuwatafutia watanzania fursa za ajira zimewezesha waalimu wa Kiswahili kupata ajira nchini Afrika ya kusini, Ethiopia na Rwanda, nafasi za madaktari 240, ajira katika bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga 16,000 na Reli ya Standard gauge 6,000. Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 idadi ya vijana   52,000 watakuwa wameajiriwa.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi