Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa maboresho yoyote ya kiutendaji yanayokwenda kufanywa kupitia uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam yatakuza biashara za ndani na nje pamoja na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani.
Ameyasema hayo leo Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba mahususi ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam.
Rais Samia amesema kuwa bandari ni moja ya kiunganishi muhimu cha kibiashara kati ya nchi yetu na mataifa mengine, kwa kuwa inahudumia shehena kubwa ya mizigo ya nchi jirani na hata mataifa ya mbali.
"Bila shaka hatua hii itaongeza mapato kwa Serikali na kuchangia kwenye uchumi wa taifa, hivyo tunaendelea kuwakaribisha zaidi wawekezaji wawekeze ili sisi tupate, nao wapate,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa, mikataba mitatu iliyosainiwa, imezaliwa kutoka kwenye makubaliano ya awali hivyo amelishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushauri wao makini na kuridhia Azimio la Makubaliano ya Awali ya Ushirikiano wa Uendeshaji wa Bandari pia amelishukuru Baraza la Mawaziri kwa kubariki mikataba hiyo iliyosainiwa.
Aidha, amewashukuru Watanzania wote walioshiriki kwa kutoa maoni kwa kila kundi pamoja na wataalam walioendesha mchakato wa majadiliano na kusisitiza kuwa hakuna kundi au sauti ambayo haikusikilizwa wala kupuuzwa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Mwenyezi Mungu aliipendelea nchi ya Tanzania kwa idadi kubwa ya watu na rasilimali za kila aina zikiwemo bandari, hivyo umasikini wa Watanzanja hauendani kabisa na upendeleo tuliopewa na Mungu ndio maana katika mipango ya Serikali, wameazimia kulipeleka taifa katika kiwango cha juu cha kati cha kipato haraka iwezekanavyo ili waweze kuwatoa Watanzania kwenye umasikini.
"Hatuwezi kuwatoa kwenye umasikini kwa kukalia rasilimali za nchi bila kuzifanyia kazi, dunia ya leo imejaa ushindani mkali, bandari yetu isipokuwa na tija, biashara itakwenda kwenye bandari za nchi nyingine, hivyo ni lazima tujizatiti, tupambane kiushindani,” alisema Dkt. Mpango.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Plasduce Mbossa ametoa shukrani kwa Rais Samia pamoja na Serikali anayoiongoza kwa dhamira ya dhati za kuhakikisha kuwa huduma za Sekta ya Uchukuzi hususani zile za bandari zinatolewa katika viwango shindani kimataifa kwa kuimarisha uendeshaji wa bandari zetu.
"Katika mikataba hii, Serikali itakuwa ikipokea ada na tozo kutoka kwa Kampuni ya DP World ambazo zitaongeza mapato yake na kupunguza gharama za uendeshaji. Kutokana na mikataba hii, Serikali itaweza kubaki na asilimia 60 ya mapato yote kutokana na gharama zote za uendeshaji kubakia kwa Kampuni ya DP World,” alimalizia Mbossa.