Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Utunzaji wa Misitu Kuongeza Uzalishaji Asali Tabora
May 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Ahmed Sagaff

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wakazi wa Tabora kutunza misitu ili kuongeza uzalishaji wa asali mkoani humo.

Akizungumza mkoani humo leo, Mheshimiwa Rais amesema Serikali haitawaruhusu tena wananchi kuchukua maeneo ya hifadhi huku akiuagiza uongozi wa mkoa huo kusimamia maeneo ambayo yametolewa kwa wananchi.

“Hatutaruhusu tena kuingia ndani ya hifadhi, maeneo ya hifadhi yana umuhimu wake, tunazungumzia hapa zao la asali, lazima tuwe na misitu ili tuweze kuzalisha asali.

“Tutakapoingia maeneo ya hifadhi tukakata misitu yote na kufanya shughuli nyingine za kibinadamu, ufugaji wa asali utakwenda wapi?” amehoji Rais Samia.

Aidha, Mkuu wa Nchi amesema dunia inanufaika kutokana na misitu hivyo ni vyema Tanzania iwe na mipango ya ardhi ili inufaike na rasilimali hiyo.

“Sasa hivi dunia ni dunia inayoingiza fedha kutokana na misitu, kuna suala la hewa ukaa, dunia inapata fedha kutokana na misitu yake iliopo, tutakapowaruhusu mvamie maeneo mkienda mkikata misitu, Tanzania haitafaidika na hii hali na ni fedha nyingi zipo huko.

“Kwenye hili la hifadhi, hatutakwenda tena kusogeza mipaka ya hifadhi na kutoa ardhi kwa wananchi, nimetoa maagizo toka juzi kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kusimamia maeneo ambayo tayari yalishatolewa,” ameeleza Mheshimiwa Rais.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi