Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Utekelezaji wa RBF Wilayani Urambo Wamvutia Waziri Ummy
Jul 18, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent - Tabora

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameipongeza Wilaya ya Urambo kwa utekelezaji mzuri wa mpango wa Malipo kwa Ufanisi (RBF) ambao umesaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Alisema baadhi ya Zahanati , Vituo vya Afya  na Hospitali ya Wilaya ya Urambo imetumia fedha kwa ajili ya upanuzi wa baadhi ya majengo na uboreshaji wa miundo mbinu jambo ambalo limewasaidia wananchi kupata huduma nzuri, bora na katika mazingira yanayovutia.

Pongezi hizo zilitolewa jana wakati akiwa katika ziara Wilayani Urambo kutembelea Hospitali ya Wilaya, Kituo cha Afya cha Ussoke , Zahanati ya Itelebulanda,  Vumilia na zahanati ya  Uyogo ili  kujionea utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na matumizi ya fedha hizo zilivyotumika kujenga majengo mbalimbali ikiwemo Wodi za Wakinamama, vyumba vya upasuaji na nyumba za waganga.

Akiwa katika Zahanati ya Itelebulanda , Mhe. Ummy aliwapongeza kwa kuweza kutumia fedha za RBF kujenga Wodi nzuri kwa ajili ya wanawake na kuahidi Wizara kuwapatia shilingi milioni 20 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu zaidi.

Alisema kazi nzuri iliyofanyika imeiwezesha Zahanati hiyo kupanda kutoka nyota moja hadi kufikia nyota tatu kwa utoaji wa huduma bora jambo ambalo ni zuri na kuwataka watumishi wake kuongeza juhudi zaidi.

Kwa upande wa Zahanati ya Uyogo alipongeza jinsi walivyotumia fedha hizo kwa ajili ya ukarabati wa jengo la huduma ya baba, mama  na mtoto, huduma ya chanjo, uzazi wa mpango, ujenzi wa choo cha watumishi na ukarabati wa nyumba za watumishi.

Alisema kuwa kutokana na Zahanati hiyo kuwa mbalimbali kutoka Hospitali ya Wilaya na kwa sababu inahudumia wananchi wengi aliahidi kuwapatia gari jipya la kubeba wagonjwa ifikapo Desemba mwaka huu.

Akiwa katika Zahanati ya Vumilia aliweza kuchangia mifuko 100 ya saruji baada ya kuona kazi nzuri ambayo imewawezesha kupanda kutoka Nyota sifuri hadi tatu kutoka na matumizi mazuri ya fedha za RBF ambazo zimewawezesha kutoa huduma nzuri ya afya kwa wakazi wa eneo hilo.

Alisema kuwa ukarabati katika jengo la wagonjwa wa nje (OPD), ukarabati wa eneo la kutupa taka, ukarabati wa vyoo vya wagonjwa na watumishi na ujenzi wa vibao vya kuelekeza wagonjwa.

Katika kituo cha Afya cha Ussoke wameweza kutumia fedha hizo za RBF kukarabati wigo unaotenganisha OPD na wodi, kukarabati chumba cha dawa na geti, kutengeneza kabati za kuhifadhia majarada na dawa, kununua samani na kukarabati mfumo wa maji safi.

Kufuatia kazi hiyo nzuri Waziri alisema Serikali itawapa milioni 40 ili waboreshe kituo hicho zaidi ili kiweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi.

Kwa upande wa Hospitali ya Wilaya kupitia RBF wameweza kukarabati jengo la wagonjwa wa nje na hvyo kuweka mazingira ya upataji huduma kwa wagonjwa kuwa mazuri.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi