Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Utangazaji Malikale, Bidhaa Asilia Wapewe Kipaumbele Katika Viwanja Vya Ndege
Oct 06, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imetoa kipaumbele kwa Watanzania kutumia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na viwanja vingine nchini kutangaza vivutio vya kitalii na utamaduni asili uliyopo hapa nchini.

Pia wametakiwa kutokuogopa ubora wa jengo la tatu la abiria, ambalo tayari limekamilika kwa asilimia 83 kuchangamkia nafasi za kufanya biashara wakati zitakapotangazwa tenda mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa kupitia kiwanja hicho.

Akizungumza katika Tamasha la Urithi Wetu lenye lengo la kuenzi utamaduni na urithi wa Mtanzania, Mhandisi Alexander Kalumbete wa TAA (pichani mwenye fulana ya njano) alisema viwanja vya ndege vina fursa nyingi ya kukuza utalii na fursa nyinginezo za kibiashara hapa nchini.

“Viwanja vya ndege vinapokea zaidi ya asilimia 60 ya watalii kwa hiyo tunaweza kutangaza vivutio vyetu kimataifa  ambavyo vinaweza kuitangaza nchi yetu na watu binafsi wanaofanya biashara za kitalii wanaweza kuja kwetu  kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na wakafuata utaratibu wa kufanya uwekezaji nao wakanufaika na utamaduni kupitia viwanja vya ndege,” alisema.

Mhandisi Kalumbete ameongeza … “Wageni wanapokuja na kuona bidhaa zetu za kiasili watanunua kwa fedha za kigeni na hii itasaidia katika ukuaji wa uchumi wa nchi”.

Mhandisi huyo alisema kukamilika kwa jengo la tatu la abiria kutatoa fursa nyingi kwa wananchi hasa wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria kwa magari binafsi wanaweza kunufaika nayo, ujenzi wa hoteli za kisasa pamoja na kufungua maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali.

“Nafasi hizi zipo kwa ajili ya Watanzania wote na serikali imesha tangaza nafasi za watu kwenda kufanya uwekezaji ndani ya Kiwanja cha ndege na kila mtu anaweza kupata eneo la uwekezaji watu wasiogope ubora wa jengo lile lipo kwa ajili yao” alisema.

Alisema katika viwanja vya ndege vingine vikiwemo vya Songwe na Mwanza ambazo uwekezaji wake unaendana na viwanda mbalimbali.

Kwa upande wake Afisa Biashara na Masoko  Mwandamizi wa TAA,  Bi. Rose Comino alisema Mamlaka hiyo inasimamia na kuendesha viwanja vya ndege 58 vilivyopo Tanzania Bara jambo ambalo linapanua wigo wa fursa kwa wananchi wanaotaka kuwekeza.

“Katika viwanja vyetu kuna fursa mbali mbali za uwekezaji kama Hoteli ya nyota nne katika kiwanja cha JNIA,  maghala ya kuhifadhi mizigo kiwanja cha Songwe,uwekezaji katika karakana za ndege, viwanda vidogo vidogo vya kuchakata samaki, maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali, chumba cha kutunza baridi (Cold room) inayotumiwa kuhifadhi bidhaa zenye kuharibika kwa muda mfupi yakiwemo maua, matunda, samaki, nyama n.k na tunakaribisha hata wafanyabiashara ndogondogo  ambao watauza bidhaa zinazoonesha utamaduni wetu.

Lengo ni kukuza uchumi wetu na kuongeza pato la Taifa. Alilisitiza kuwa Mamlaka inaendelea na itaendelea kuboresha viwanja vya ndege zaidi” alisema.

Pia, Alisema usalama wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndege nchini imeimarishwa kwa kiasi kikubwa ikiwemo kufungwa mitambo ya kisasa ya kiusalama.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi