Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaahidi wakazi wa Wilaya ya Mkalama kwamba Serikali itaipa kipaumbele wilaya hiyo pindi itakapotangaza ajira za Walimu.
Akizungumza leo mkoani Singida, Rais Dkt. Samia amesema hatua hiyo itashughulikia changamoto ya upungufu wa Walimu aliyoelezwa leo na wawakilishi wa wananchi katika wilaya hiyo.
"Katika wilaya hii, takwimu zinaonesha kwamba kwa shule za msingi kuna upungufu wa Walimu kwa zaidi ya asilimia 40, na shule za sekondari asilimia 26, kwa hiyo tutakwenda kuifanyia kazi changamoto hii," ameahidi Mkuu wa Nchi.
Naye, Mbunge wa Iramba Mashariki, Mhe. Francis Isack amemuomba Rais Dkt. Samia awajengee kituo cha afya, barabara na awawekee tenki la maji ili kuongeza huduma za kijamii katika wilaya hiyo, ambapo Serikali imefanikiwa katika kufikisha huduma mbalimbali.
Tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021 Rais Samia amekuwa akiimarisha sekta ya elimu kwa kuongeza idadi ya madarasa, idadi ya Walimu na kuanzisha juhudi za kubadilisha mtaala ili uzalishe wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri.