Na Shamimu Nyaki - Dodoma
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameeleza kuwa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu jijini Dodoma upo katika hatua ya utekelezaji na tayari Serikali imeshaanza kutenga fedha za ujenzi huo.
Mhe. Gekul ameeleza hayo leo Septemba 13, 2022 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge, Mhe. Innocent Edward Kalogeris (Morogoro Kusini) aliyeuliza ni lini ahadi ya ujenzi wa Uwanja wa mpira Dodoma iliyotolewa na Mfalme wa Moroko itatekelezwa.
Akijibu swali hilo, Mhe. Gekul amesema, mawasiliano kuhusu utekelezaji wa mradi huo baina ya Serikali ya Tanzania na Morocco yanaendelea, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau na wabia wa maendeleo.
"Serikali imeshakamilisha upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi huo, na mwaka huu wa fedha ujenzi utaanza lakini pia kutakua na kiasi cha Shilingi bilioni 10 kuboresha viwanja vya michezo vya Arusha, Tanga, Dodoma na Geita", amesema Mhe. Gekul.
Mhe. Waziri wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa ametoa majibu ya nyongeza katika swali hilo kwa kusisitiza kuwa ujenzi huo utakua wa kisasa na miondombinu bora ambayo inaendana na teknolojia ya viwanja vya sasa Duniani.
Akijibu swali la nyongeza la Mhe.Salma Kikwete kuhusu kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa Majaliwa Stadium, Mhe. Gekul amesema Serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za wadau wanaowekeza katika Sekta ya michezo ambapo amesema imepunguza kodi katika nyasi bandia pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wawekazaji wa sekta hiyo.
Mhe. Gekul ametumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa ujenzi wa Uwanja wa Ruangwa na kueleza kuwa ujenzi huo utakua chachu ya kuongeza vipaji katika Soka, na kupunguza changamoto ya miundombinu ya viwanja nchini.