Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema uongozi sio kubadilisha watu uliowakuta badala yake ni kujenga ushawishi wa kubadili mitazamo ya wale unaowaongoza kwa kuonesha njia ili kufikia malengo makubwa ya kuwahudumia wananchi.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa Njia ya Mtandao Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne inayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aalto cha nchini Finland.
Mhe. Simbachawene amesema kuna tabia imejengeka kwa baadhi ya viongozi mbalimbali nchini pindi wanapopewa uongozi huanza kuwaondoa baadhi ya Watumishi waliowakuta katika Ofisi za Umma kwa kisingizio kuwa hawaendani na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza kuwa, Kiongozi bora hahitaji kujitambulisha kuwa yeye ni nani bali hutambuliwa kwa jinsi anavyojiweka na anavyoendesha mambo yake kwa wale anaowaongoza.
''Ukiona kiongozi anajitambulisha kuwa yeye ni nani tambua kuwa hapo kuna walakini, kiongozi hutambuliwa na watu kwa jinsi anavyojiweka katika jamii kwa matendo yake mema yanayozingatia maadili'', amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Akizungumzia Programu hiyo ya uongozi ngazi ya cheti, Mhe. Simbachawene amewataka washiriki kusoma kwa bidii kwani Programu hiyo ni muhimu kwa vile inalenga kuisaidia Serikali katika kuimarisha utendaji kazi na hatimaye kuwaletea wananchi maendeleo.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha utawala bora, nidhamu, uwajibikaji na maadili katika kada zote za uongozi.
Amesema mafunzo hayo yamehusisha washiriki kutoka sekta ya umma na sekta binafsi ambao kimsingi jukumu lao kuu ni moja ambalo ni kuhudumia wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na haki.
Mhe. Simbachawene amewahimiza washiriki kuzingatia mafunzo hayo ili yakawe nyenzo muhimu ya kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi wao na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na hatimaye kuwa na utawala bora wenye kuzingatia sheria, maadili na haki.
Kwa upande wake Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting ameisifu Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kwenye suala la uongozi hususan, kwenye idadi kubwa ya wanawake ambao ni viongozi wakubwa kwenye sekta ya umma na binafsi.
''Kwa mwelekeo huu, mimi kama Balozi nitaendelea kuishawishi nchi yangu kuendelea kufadhili Taasisi ya UONGOZI ili kuibua wanawake wengi zaidi katika ngazi za juu za maamuzi'', amesema Mhe. Balozi.
Awali, Mtendaji Mkuu, Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema Taasisi yake imejielekeza kuandaa viongozi wenye maarifa na wanaojua wajibu wao kwa wanaowangoza na wananchi na sio wanaotaka kupata vyeti tu.
Jumla ya washiriki takriban 70 kutoka sekta ya umma na sekta binafsi wanashiriki programu ya mafunzo hayo yatakayofanyika kwa muda wa miezi sita.