[caption id="attachment_53296" align="aligncenter" width="768"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wengine mara baada ya kuwasili kwa Ndege mpya aina ya Boeng 787-8 Dreamliner ambayo imenunuliwa na Serikali. (Picha kutoka Maktaba)[/caption]
Na Jacquiline Mrisho – Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa baada ya kufufua Shirika la Ndege (ATCL) na kununua ndege mpya 11 idadi ya wasafiri wa anga nchini imeongezeka kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 5.8 mwaka 2018.
Rais Magufuli ametoa takwimu hizo jana Bungeni, jijini Dodoma wakati akilivunja Bunge la 11 ambapo amesema kuwa kati ya ndege 11 zilizonunuliwa, ndege 8 tayari zimeshawasili na zinafanya kazi.
Amesema kuwa pamoja na wasafiri kuongezeka, faida nyingine ya ndege hizo zimeonekana katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.
“Kwa kutumia ndege zetu tumeweza kuwarejesha Watanzania wenzetu waliokwama nchi mbalimbali kutokana na kusitishwa kwa usafiri wa anga katika mataifa mbalimbali ikiwa ni njia moja wapo ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa huu, kama tusingekuwa na ndege zetu tungeshindwa”, alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia kuhusu usafiri wa anga, Rais Magufuli ameelezea kuwa ujenzi wa jengo jipya la Abiria (Terminal III) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere umekamilika wakati upanuzi wa Viwanja vya Kimataifa vya Kilimanjaro (KIA) na Abeid Aman Karume kule Zanzibar unaendelea.
Vilevile, ujenzi wa viwanja vingine 11 upo katika hatua mbalimbali na Serikali ipo mbioni kumpata mkandarasi wa kujenga Uwanja wa Kimataifa wa Msalato hapa Dodoma.
Aidha, Serikali pia imekamilisha ujenzi wa rada ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza, ujenzi wa Songwe/Mbeya unakaribia kukamilika.