Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

UNICEF Yaipongeza Zanzibar Utoaji Huduma kwa Watoto
May 03, 2019
Na Msemaji Mkuu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto Duniani (UNICEF) limepongeza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwahudumia watoto ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya na elimu.

Mwakilishi wa UNICEF katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaemaliza muda wake wa kazi Bi Maniza Zaman aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Mwakilishi huyo  wa UNICEF ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuwahudumia watoto sambamba na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo kupata elimu na afya bora.

Alieleza kuwa Shirika hilo linathamini juhudi hizo na limeweza kushuhudia mafanikio na mabadiliko makubwa katika sekta za maendeleo hatua ambazo zimewawezesha watoto wa Zanzibar na wao kuweza kupata haki zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu ya kimaisha.

Bi Zaman alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake hizo na kueleza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana katika sekta ya afya ni pamoja na kupungua kwa vifo vya akina mama na watoto kwa kiasi kikubwa hapa Zanzibar.

Aidha, Mwakilishi huyo alimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake kubwa anazozichukua katika kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto, maradhi mbali mbali yakiwemo kipindupindu, Malaria na mengineyo huku akiahidi Shirika hilo kuendelea kuisaidia sekta hiyo hapa nchini.

Mwakilishi huyo alieleza kuwa UNICEF itaendelea na programu mbali mbali hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na zile za kusaidia jamii hasa watoto mjini na vijijini sambamba na kuwawezesha kiuchumi.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake amelipongeza Shirika la UNICEF kwa juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kumpongeza Mwakilishi wa Shirika Bi Zamani kwa utendaji wake mzuri wa kazi katika kipindi chake chote alichokuwepo Tanzania.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Shirika la UNICEF lina historia kubwa na mashirikiano kati yake na Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo sekta ya afya, elimu sambamba na kuimarisha ustawi wa akinamama na watoto hapa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Shirika hilo limeendelea kutoa ushirikiano na msaada mkubwa kwa watoto wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu kadhaa ambazo zimeweza kusaidia katika kuleta maendeleo endelevu kwa watoto na jamii kwa ujumla.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kupambana na vifo vya akinamama na watoto, ambapo Zanzibar imepiga hatua kubwa hasa pale ilipoanzisha mapambano dhidi ya Malaria jambo ambalo limefanikiwa.

Rais Dk. Shein aliupongeza uongozi huo wa (UNICEF) nchini Tanzania na kueleza kuvutiwa kwake na mikakati pamoja na programu mbali mbali zilizowekwa na Shirika hilo katika kuhakikisha linaendelea kuwasaidia watoto katika nyanja mbali mbali.

Alieleza kufurahishwa na mipango kabambe iliyowekwa na Shirika hilo katika kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika nguzo zake nne ilizoziweka ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya kwa watoto, ukatili dhidi ya wanawake na watoto,kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuunga mkono Mpango wa Maendeleo endelevu (SDG).

Aidha, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo wa (UNICEF) hapa nchini anaemaliza muda wake mikakati madhubuti iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea Mapinduzi ya Januari 12, 1964 katika kuhakikisha inaimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu na sekta ya afya ambazo zote kwa pamoja zina dhima kubwa katika kuwaendeleza na kuwahudumia watoto wa Zanzibar.

Alisema kuwa katika sekta zote mbili za afya na elimu tayari Serikali imeshatangaza kuwa huduma za afya kwa wananchi ziwe bure kama ilivyokusudiwa katika malengo ya Mapinduzi sambamba na sekta ya elimu ambapo kwa elimu ya msingi na sekondari zote ni bure.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuzisimamia vyema, Sera, Kanuni na Sheria zinazowahusu watoto katika kupata haki zao za msingi na huduma za kijamii sambamba na kuahidi kuendelea kushirikiana na Mashirika ya Umaoja wa Mataifa likiwemo Shirika la (UNICEF).

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi