Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Unicef Kuisaidia Serikali Kufanya Tafiti za Maendeleo ya Mtoto
Oct 24, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: WFM - Dodoma

Shirika la Umoja wa Mataifa  la Kuhudumia Watoto ( UNICEF), wameonesha nia ya kuisaidia Serikali ya Tanzania kufanya tafiti mbalimbali kuhusu maendeleo ya mtoto ili kukabiliana na changamoto zinazomkabili.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, baada ya mkutano wake na Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Leila Pakkala, uliofanyika ofisi za Wizara hiyo Jijini Dodoma.

Dkt. Mpango alisema kuwa Shirika la UNICEF, lina nia yakushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ili kuweza kufanya tafiti katika mikoa mbalimbali, kuzichapisha na kuzisambaza ili kuongeza uelewa wa watu kuhusu  maendeleo ya watoto.

“Watu wengi wanajua uwekezaji kwa maana ya barabara na miundombinu mingine mikubwa lakini katika mazungumzo yetu tumesisitiza kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya watu hasa katika umri mdogo kwa kuwa usipowekeza katika umri huo na kuwekeza katika umri mkubwa matokeo yake hayawi mazuri.”, alisema Dkt. Mpango.

Alisema kuwa, maeneo ambayo ni muhimu kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na UNICEF ni pamoja na udumavu, elimu kwa ajili ya watoto hasa ambao hawajafikia umri wa kwenda shule na sheria ya mtoto katika kuhakikisha anakua salama kwa lengo la kulitumikia taifa kwa siku za usoni, hivyo alisisitiza kuwekeza  mapema kwa mtoto katika afya, lishe, elimu, uhuru wao na usalama hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kulitumikia Taifa kwa wakati ujao.

Aidha Dkt. Mpango alisema kuwa,  Serikali inafanya  jitihada kubwa kusimamia maendeleo ya uchumi kwa ujumla,  kwa kuwa Taifa lisipokuwa na uchumi imara haliwezi kuwekeza katika maendeleo ya watoto.

Alisema bajeti zinatakiwa kuweka umuhimu wa kuwekeza katika mtoto hivyo kuna Kitengo kinachohakikisha bajeti ya Serikali Kuu na Halmashauri zinazingatia mambo ya msingi ambayo yatasaidia watoto wa Tanzania kuwa na maendeleo stahiki.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Leila Pakkala, amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika maendeleo ya mtoto jambo ambalo linastahili pongezi na pia ameipongeza Serikali kwa ukuaji wa uchumi, kupambana na rushwa, ujenzi wa miundombinu na kuongeza mapato ya ndani kupitia kodi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto- UNICEF,  kwa juhudi zinazofanywa kuhakikisha maendeleo ya mtoto nchini Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla kwa kuwekeza katika lishe na elimu ili kuwa na kizazi kijacho chenye uelewa wa kutosha ili kuleta tija katika Sekta za Maendeleo.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha ya Mipango

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi