[caption id="attachment_8519" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpa mkono Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni baada ya kumaliza kuhutubia katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga Nchini Tanzania.[/caption]
Na. Paschal Dotto na Thobias Robert-MAELEZO
Hali nzuri ya ulinzi na usalama imetajwa kuwa kichocheo cha Ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kupita nchini Tanzania. Bomba hilo litajengwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Jijini Tanga.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika uzinduzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi jiji tanga.
“Mheshimiwa Museveni nakuhakikishia Tanzania iko imara, usalama wa bomba hili ni wa uhakika mimi nafahamu katika kuchambua kwako ndiyo maana ulichagua bomba hili lipite Tanzania kwa sababu unaamini ulinzi wa Tanzania ni mzuri,” alisema Rais Magufuli.
Mradi huo utakaokuwa na kilomita 1115 kwa upande wa Tanzania na kilomita 330 upande wa Uganda utapita katika mikoa 8, wilaya 24 pamoja na vijiji 128. Mikoa itakayopitiwa na bomba hilo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Dodoma na Tanga.
[caption id="attachment_8521" align="aligncenter" width="750"] Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipeana mkono na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga Nchini Tanzania[/caption]Kwa upande wake Rais Museveni wa Uganda alisema kuwa waafrika waungane katika kujiletea maendeleo badala ya kutegemea mataifa ya kigeni.
“Tutapata petrol, dizeli, mafuta ya taa na mafuta ya ndege ili sasa na sisi ndege zetu zipate mafuta kutoka kwetu kwa bei nafuu na Uganda tutafufua shirika letu la ndege,”alisema Rais Museveni.
Aidha, Rais Museveni alisema kuwa hakuna mtu wa kuzuia kukua kwa maendeleo katika nchi hizi kwa sababu fedha zitakazotokana na bomba hili zitasaidia kujenga miundo mbinu mingine bila kutegemea mikopo kutoka nje ya nchi.
Akiongea mapema, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassani amsema kuwa mradi huu utaongeza ushirika wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili.
Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medadi Kalemani alisema kuwa ujenzi wa bomba hilo utakaogharimu zaidi ya dola za kimarekani billioni 3.5, unatarajia kuzalisha faida mbalimbali kama vile ajira,nyumba za kulala wageni na umeme wa megawati 35 kwa maeneo yote bomba litakapopita.
[caption id="attachment_8522" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati wa Uganda Irene Muloni akiongea eneo la Chongoleani Jijini Tanga wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga Nchini Tanzania.[/caption]“Mradi huu ni uwekezaji mkubwa kwa sababu maeneo yote yatakayopitiwa na mradi huu yatajenga fursa za kiuchumi, viwanda na maendeleo mengine ya kisayansi na teknolojia,” amsema Dkt. Kalemani.
Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini, Mhandisi Irene Muloni amesema kuwa mradi huo una faida kwa Afrika Masharika na si Tanzania na Uganda pekee ambapo pia utaongeza wawekezaji kwa asilimia 55.
Aidha, mradi utawezesha upanuzi wa bandari ya Tanga ili Tanzania iwe na bandari tatu kubwa nyingine zikiwa ni Dar es Salaam na Mtwara, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira 10,000 wakati wa ujenzi na ajira za kudumu 1,000 baada ya ujenzi kukamilika.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema kuwa wataulinda mradi huo kwa faida ya nchi hizi mbili na wanawakaribisha wageni kuwekeza katika makazi na watahamasisha ofisi mbalimbali kujengwa katika eneo la mradi.
Ujenzi wa mradi huu utaanza rasmi januari 2018 unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 ambapo unajengwa na kampuni za TOTALE na CNOOC za nchini Ufaransa na TULLOW ya Uingereza. Kwa upande wa Tanzania mradi utasimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa niaba ya Serikali.