Na Mbaraka Kambona,
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kusafirisha Mizigo (DHL) nchini Tanzania, Bi. Fatma Abubakar kujadiliana namna Serikali na shirika hilo watakavyoweza kushirikiana kufungua zaidi masoko ya Kimataifa ya zao la Dagaa na Mwani.
Waziri Ulega alikutana na Mkurugenzi Mtendaji huyo wa DHL jijini Dodoma Mei 19, 2022.
Akizungumza katika majadiliano yao hayo, Waziri Ulega alisema zao la dagaa kwa muda mrefu limekuwa likiuzwa katika nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Amerika lakini biashara hiyo imekuwa ikifanywa kienyeji sana jambo ambalo limesababisha nchi na watu wake kutokuona tija kubwa ya zao hilo.
"Pamoja na dagaa kuuzwa katika masoko ya nje bado watu wanafanya kienyeji sana, tunatakiwa tuwekeze katika kuliongezea thamani zao la dagaa na kulifungasha vizuri ili liweze kuthaminika katika masoko ya kimataifa na litanunuliwa kwa wingi kuliko ilivyo hivi sasa", alisema.
Aliongeza kwa kusema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na dagaa kwa wingi kuanzia baharini na katika maji baridi isipokuwa bado halijawekewa mnyororo wa thamani mzuri ili kulipa heshima yake na kuweza kuwainua wananchi.
"Tuweke mipango mizuri ya masoko ya dagaa na mwani ili kusudi tuweze kuona namna tunavyoweza kushirikiana katika kuyaboresha mazao hayo na kuyatafutia masoko ya uhakika nje ya nchi", alifafanua
Alisisitiza kwa kusema kuwa ni muhimu sasa zao la dagaa likapata hadhi yake, mnyororo wa thamani wa zao hilo uimarishwe ili Wafanyabiashara waondokane na uuzaji wa dagaa katika magunia na waanze kuwaweka katika vifungashio vizuri vitakavyovutia biashara ya kimataifa.
Aidha, alisema ni muhimu kuanza kuelimisha Vikundi vya Ushirika vya Uvuvi ambavyo tayari vipo kwani kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kuwafikia Wafanyabiashara hao na kuwaelekeza namna ya kuboresha biashara zao ili ziweze kukidhi masoko ya kimataifa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Kusafirisha Mizigo (DHL), Bi. Fatma Abubakar alisema kuwa walianza kuwawezesha Wafanyabiashara wa dagaa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika lakini wanakusudia kuupeleka mradi huo pia mkoani Mwanza ili Wafanyabiashara mkoani humo waweze kujua namna ya kufanya ili waweze kuuza dagaa wao nje ya nchi.
"Kwa upande wetu sisi tunapenda tufanye kazi pamoja ili tuweze kuwasaidia wafanyabiashara wetu wa Tanzania na waweze kujikimu kimaisha", alisema Abubakar
Kuhusu zao la Mwani, Abubakar alisema kwa sasa wameanzisha mradi wa kuwawezesha wakulima wa mwani waliopo Visiwani Zanzibar na wanategemea kuendelea kuwaelimisha ili zao hilo liweze kuwafaidisha zaidi.