[caption id="attachment_6193" align="aligncenter" width="750"] Msanii wa Filamu nchini Issa Mussa maarufu kama Clod 112 (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitambulisha filamu yake mpya ijulikanayo kama “Tusijisahau,” katikati ni Mtayarishaji wa filamu hiyo Bi. Amina Musa na kushoto ni Mwakilishi toka Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Esther Ibrahim.[/caption]
Na Agness Moshi
Msanii wa filamu za kitanzania Bwana. Issa Mussa maaarufu kama Cloud 112 amesema kuwa filamu za kitanzania hazijashuka thamani kama inavyodaiwa na watu wengi bali ukosefu wa ubunifu ndiyo unapelekea kuonekana kushuka kwa soko la filamu hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Cloud 112 wakati wa mkutano na waandishi wa habari wakati akitambulisha filamu yake mpya ijulikanayo kama “Tusijisahau” iliyofanyika nchini Sweden.
Cloud amesema kuwa filamu za kitanzania bado zina thamani na si kweli kuwa zimeshuka thamani kama inavyodaiwa, japo wasanii bado wanakumbana na changamoto ya kipato inayopelekea kushindwa kutengeneza filamu zenye ubora na viwango vinavyotakiwa.
“Kipato ni moja ya changamoto inayosababisha kushuka kwa filamu za kitanzania kwani msanii hawezi kutengeneza filamu nzuri kama hana uhakika wa kula chakula na kupata mahitaji mengine ya msingi,” alisema Cloud.
Aidha Cloud aliongeza kuwa wasanii wa filamu za kitanzania wanaweza kutengeneza filamu nzuri kama wakiwezeshwa kwa kipato kwani ndiyo changamoto kubwa inayoikabili tasnia ya filamu nchini.
[caption id="attachment_6196" align="aligncenter" width="750"] Mtayarishaji wa filamu ya “ TUsijisahau” Bi. Amina Musa (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakitambulisha filamu hiyo mapema hii leo jijini dare s Salaam, katikati ni Muigizaji wa filamu hiyo Bw. Issa Mussa maarufu kama Clod 112 na kulia ni Mhasibu wa kampuni ya AMUS Entertainment Bw. Abdul Vencha. (Picha na Eliphace Marwa )[/caption]“Filamu hii itakua ni ya tofauti kwani imefanyika nje ya mipaka ya Tanzania, inasisimua , imetumia mwongozo ulionyooka bila kupoteza muda, yenye ubora na imewapa watanzania wanachohitaji kwa sababu waandaji wamefanya tafiti kabla ya kutengeneza filamu hii,” alisema Cloud.
Aidha msanii huyo alitoa pia ombi kwa serikali kuhusiana na sheria ya filamu ambayo ina wakandamiza wasanii hususani kwenye tasnia ya filamu.
“Ninaomba serikali itubadilishie sheria ya filamu kwani kwa sasa kumekuwa na wimbi la maharamia ambao huiba kazi za wasanii na hata adhabu zake pale haramia anapokamatwa inakuwa ni ndogo ukilinganisha na hasara aliyopata msanii,” alisema clouds.
Naye mwakilishi kutoka Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Esther Ibrahim aliyeambatana na msanii huyo amewataka watanzania kutoa ushirikiano kwa wasanii wa filamu nchini kwa kununua na kuangalia kazi zao ili waweze kujifunza.
“Naomba nitumie fursa hii kuwataka Watanzania kutoa ushirikiano kwa wasanii wa nyumbani kwa kununua kazi zao ili waweze kufanya kazi nzuri ambazo zitaweza kuvuka mipaka kama alivyofanya ndugu yetu Cloud,” alisema Bi. Esther.
Filamu hiyo ya Tusijahau inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi oktoba mwaka huu ikiwa na lengo la kufundisha watanzania kuhusu picha halisi ya maisha ya Ulaya ili waweze kuachana na mawazo ya kuwa shida zipo tu Tanzania.