Ukarabati wa kivuko cha MV. KAZI kinachofanya safari zake kati ya Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 80 ambapo mwezi ujao kinatarajiwa kurejea kuanza kutoa huduma. Kivuko hicho kiliondolewa rasmi kwenye maji mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu baada ya kufikia muda wake wa ukarabati ambapo ni miaka mitatu hadi mitano tangu kianze kutoa huduma.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala mwishoni mwa wiki hii wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Yadi ya Songoro Kigamboni jijini Dar es Salaam ambapo kivuko hicho kinaendelea kufanyiwa ukarabati.
“Tumefanya ukaguzi wa mwisho takriban mwezi mmoja uliopita, kikubwa kilichokuwa kinasubiriwa ilikuwa ni vifaa, kwa sababu ile kazi sehemu kubwa ilikuwa ni kufunga vifaa vipya vya injini, gia boksi, na mifumo mipya ya injini, kwahiyo zile kazi ambazo zilikuwa zinaweza kufanyika kabla ya vifaa hivyo ilikuwa zaidi ya asilimia themanini na zote zilifanyika ikiwemo kazi za kuondoa vipande vya bati ambavyo vimeharibika na kupiga rangi upya”. Alisema Mtendaji Mkuu.
Awali, Mwakilishi wa kampuni ya Songoro Marine wanaofanya ukarabati wa kivuko hicho Hamad Aweso amesema ukarabati wa kivuko hicho umefikia hatua nzuri na amebainisha kuwa kuna vifaa ambavyo vilichelewa kufika kwa wakati zikiwemo injini za kivuko hicho na kwa sasa vifaa hivyo vimeshafika hivyo kazi iliyobaki ni kuvifunga ili kivuko kiweze kurejea kutoa huduma.
“Kwa sasa hivi zoezi linaloendelea ni la kufunga hizi injini na kwa hali inavyoendelea tunategemea mwisho wa mwezi wa kumi na moja zoezi zima litakuwa limekamilika na chombo kitakuwa kimekwishaingizwa majini, alimaliza mkandarasi huyo.
Kivuko cha MV. KAZI kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 sawa na tani 170 na tangia kuondolewa kwa kivuko hicho, eneo la Magogoni Kigamboni limebakia na vivuko viwili ambavyo vinatoa huduma kikiwemo kivuko cha MV. MAGOGONI na MV. KIGAMBONI ambavyo kwa sasa vinasaidiana na vivuko viwili kutoka kampuni ya Azam Marine kutoa huduma eneo hilo.