Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujerumani Yatoa Msaada wa Bilioni 330 kwa Ajili ya Mradi wa Maji Simiyu
May 03, 2019
Na Msemaji Mkuu

Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo (KfW) imeipatia Tanzania ruzuku ya Euro milioni 127.7, sawa na sh. bilioni 330, kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria katika mkoa wa Simiyu.

Makubaliano ya msaada huo kupitia mikataba miwili yamesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani, (KfW) anayeshughulikia nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya, Dkt. Klaus Mueller.

Katika mkataba wa kwanza, kiasi cha Euro 102.7, sawa na shilingi bilioni 265 kimetolewa na Mfuko wa Kimataifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi (Green Climate Fund) na mkataba wa pili unahusisha Euro milioni 25, sawa na sh. bilioni 65 ambazo zimetokelewa na Benki ya Maendeleo ya UJerumani (KfW).

Mbali na mradi wa maji  wa Simiyu ambao chanzo chake cha maji ni kutoka Ziwa Victoria, miradi mingine itakayonufaika na msaada huo ni kilimo endelevu cha umwagiliaji, usafi wa mazingira, maji na malisho ya mifugo na kuzijengea uwezo taasisi zitakazotekeleza mradi huo hasa mamlaka za maji katika Wilaya tano za Bariadi, Itilima, Meatu, Busega na Maswa zitakazonufaika na mradi huo.

"Kutokana na umuhimu wa mradi huo wa maji, Serikali kwa upande wake itachangia Euro milioni 40.7 sawa na sh. bilioni 104 na wananchi watakao nufaika na mradi huo watachangia Euro milioni 1.5 sawa na sh. bilioni 3.8 na kufanya gharama za mradi mzima kufikia zaidi ya Euro milioni 171 sawa na zaidi ya sh. bilioni 446" alisema Bw. Doto James

Aliishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia Mfuko wake wa Kimataifa wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (GCF) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha fedha kitakachotumika kutekeleza mradi huo utakachukua miaka mitano hadi kukamilika kwake.

"Katika kipindi cha miaka  mitatu Serikali ya Ujerumani imeipatia Tanzania zaidi ya Euro 202.8 sawa na shilingi bilioni 518.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya, nishati, uhifadhi wa maliasili, udhibiti wa fedha za umma na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi" alisisitiza Bw. James

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya KfW amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Mfuko wa Kimataifa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kutoa kiasi kikubwa cha fedha cha Euro milioni 102.7 kwa mkupuo katika nchi za kiafrika tangu mfuko huo uanzishwe.

"Tunaamini kuwa zaidi ya watu 500,000 watanufaika na mradi huu wa maji kutoka Ziwa Victoria unaohusiana na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kutuhifadhi vyanzo vya maji, usafi wa mazingira, kuendesha kilimo bora chenye kuhifadhi mazingira" aliongeza Dkt. Mueller.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo, amempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuipatia Wizara yake zaidi ya shilingi trilioni 3 katika kipindi kifupi cha miaka mili kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji inayoendelea kujengwa nchini kote.

Alitaja sababu za mkoa wa Simiyu kunufaika na msaada huo kuwa ni mkoa unaokabiliwa na hali mbaya ya hewa ukiwemo ukame na kwamba mradi huo utawawezesha wananchi kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kwamba katika ukanda huo wa Ziwa kutakuwa na miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.2 itakayokuwa inatekelezwa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Mahamoud Mgimwa amesema Bunge litahakikisha linausimamia mradi huo utekelezwe kwa wakati kwa sababu Serikali imedhamiria kwa dhati kuona kwamba wananchi wanapata maji safi na salama kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi