[caption id="attachment_37227" align="aligncenter" width="749"] Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Dkt Detlef Waechter[/caption]
Na: Judith Mhina - MAELEZO
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Dkt Detlef Waechter amempongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kufanikiwa kupambana na rushwa nchinI Tanzania na kupata mafanikio makubwa ndani ya kipindi kifupi.
Hayo amesema Balozi Waechter alipofanya mahojiano na Idara ya Habari-MAELEZO mapema jana katika hoteli ya Hyatt Regency The Kilimanjaro Dar-es-salaam Kempinski katika barabara ya Sokoine Jijini Dar-es –salaam.
Akielezea jinsi rushwa ilivyoota mizizi sehemu nyingi ikiwemo Ujerumani amesema “Tatizo la rushwa sio la Tanzania peke yake, hata kule Ujerumani lipo japo si kwa kiasi kikubwa kila mara Serikali inapaswa kujiangalia na kuhakikisha inapambana na “mfumo wa rushwa mahala popote Ili wananchi wawe na imani na serikali yao.
Kwa dhati kabisa nampongeza Rais Magufuli kwani hali ilikuwa sio nzuri kulingana na ripoti tuliyoisikia wakati wa Mkutano wa 38 wa Bara la Afrika wa Kuthibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya miezi mawili iliyopita. Uwepo wa rushwa Tanzania ilikuwa ni eneo linalotumiwa katika kupitisha dawa za kulevya lakini hivi sasa suala hili limepungua kwa kiasi kikubwa kutokanana juhudi za Rais Magufuli”, alieleza Balozi Waechter.
Akielezea ubaya wa rushwa, Balozi Waechter amesema kuwa matatizo ya rushwa yanarejesha nyuma maendeleo kwa kuwa watu hawapati huduma wanazostahili kwa kuwa tu kuna wengine wanatumia rushwa na kwamba uwepo wa rushwa unaondoa uaminifu kutoka Taifa moja kwenda linguine.
Anasema maeneo ambayo hayana utulivu na amani mara nyingi husababishwa na kushamiri kwa rushwa na kwamba na Serikali ambazo hazisimamii vema huduma kwa wananchi wake.
“Raia kutoka nchi za Afrika wanakwenda Ulaya sio kwa kupenda bali ni kwa sababu wamekosa utulivu na amani katika nchi zao, kinachopatikana nchini kwao ni kwa ajili ya wajanja wachache wanaoweza kutoa rushwa na kuhodhi utajiri wa nchi badala ya kuhudumia wananchinwote”, ameeleza Balozi Waechter.
Pia Balozi Waechter ameelezea kufurahishwa na Tanzania kuona umuhimu wa viwanda katika kujenga uchumi wa nchi ya Tanzania kwani haiwezekani nchi ikazalisha malighafi halafu itegemee nchi nyingine inunue kwa ajili ya kutengenza bidhaa halafu ziuzwe tena kwa nchi iliyotoa malighafi.
“Nadhani ni uamuzi wa busara kabisa Tanzania imefanya kuelekea katika nchi ya uchumi wa viwanda”, aliongeza.
Ameeleza kuwa nchi zote zilizoendelea kama Ujerumani zimefika zimepata maendeleo baada ya kufanya mageuzi ya hali ya juu katika suala zima la viwanda na tekinolojia. Amesema Ujerumani ipo tayari kushirikiana na Tanzania pale ambapo itahitajika katika kuendeleza juhudi za kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,
Akielezea suala zima la nchi zote mbili kujifunza kutoka kwa mwenzake, Balozi huyo amesema kuwa Ujerumani inajifunza kitu kikubwa sana hapa Tanzania ambacho chimbuko lake ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere suala zima la Amani na Utulivu ambao anasema yeye binafsi hajawahi kuona sehemu yeyote ambayo aliweza kuishi.
Tanzania na Ujerumani zimekuwa na uhusiano mzuri na kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.