Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujerumani Yaipatia Tanzania Msaada wa Shilingi Bilioni 23.7
Aug 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani zimetiliana saini mkataba wa msaada wenye thamani ya Euro milioni 10 sawa na Shilingi bilioni 23.7 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa kukabiliana na migongano kati ya wanyamapori na binadamu, Mradi wa kuwezesha upatikanaji wa haki za wanawake na watoto na Mradi wa kuandaa maandiko ya kitaalamu ya miradi.

Mkataba huo umesainiwa jijini Dar es Salaam, kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe. Regine Hess kwa niaba ya Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Tutuba alisema kuwa Mradi wa kukabiliana na migongano kati ya wanyamapori na binadamu umetengewa kiasi cha Euro milioni 6 ambacho kitatumika kupunguza vifo vinavyosababishwa na wanyamapori kwa jamii zinazozunguka baadhi ya hifadhi za wanyamapori na kuepusha uharibifu wa bayoanuai katika hifadhi za wanyamapori.

Bw. Tutuba aliongeza kuwa Mradi wa kuwezesha upatikanaji wa haki za wanawake na watoto utatekelezwa kwa kiasi cha kwa Euro milioni 3 ambacho kitachangia kuboresha upatikanaji wa haki za wanawake na watoto.

“Utekelezaji wa mradi huu utasaidia kuondoa ubaguzi wa kijinsia na unyanyasaji kwa wanawake na watoto na kuongeza usawa wa kijinsia nchini”, alisema Bw. Tutuba.

Aidha, alisema kuwa, Mradi wa tatu ni kwa ajili ya kuandaa maandiko ya kitaalamu ya miradi, ambapo kiasi cha Euro milioni 1, zitatumika kufanya pembuzi yakinifu za miradi inayotekelezwa kwa fedha za misaada kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.

“Msaada huu ni sehemu ya ahadi ya misaada ya jumla ya Euro milioni 71 sawa na Shilingi bilioni 188.65iliyotolewa na Shirikisho hilo, katika majadiliano yaliyofanyika baina ya pande hizi mbili, jijini Dar es Salaam tarehe 25 Novemba, 2021 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo”, alifafanua Bw. Tutuba.

“Nawahakikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, itafuata taratibu na kanuni zote za kisheria na kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa”, aliongeza Bw. Tutuba.

Bw. Tutuba amemshukuru Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regine Hess kwa niaba ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani kwa msaada huo mkubwa.

Kwa Upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe. Regine Hess, amesema kuwa Serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu, aliahidi kusimamia fedha hizo ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Bw. Juma Selemani Mkoni, alisema kuwa Wizara hiyo imekua ikinufaika na misaada mbalimbali kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani ambapo kwa kipindi cha miaka mitano (2017 -2022) wizara hiyo imepokea kiasi cha Sh.  Bilioni 350.

Tanzania imenufaika na misaada kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani katika maeneo mbalimbali ikiwemo Sekta ya maji, Sekta ya nishati, matumizi endelevu ya maliasili na utunzaji wa mazingira, usimamizi bora wa fedha za umma na fedha za kuandaa maandiko ya miradi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi