Naibu Waziri (Afya) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kusimamia miradi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya ili vikamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha na kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi haraka iwezekanavyo.
Naibu Waziri Dkt. Dugange ametoa agizo hilo leo (Januari 1, 2024), wakati wa kikao kazi baina yake na watendaji wa Idara ya Afya Ofisi ya Rais-TAMISEMI kilichofanyika Jijini Dodoma kikiwashirikisha pia watendaji wa Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya pamoja na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchi nzima kwa njia ya mtandao.
Katika kikao hicho Dkt. Dugange amesema ni lazima watendaji katika sekta ya afya wakiri kuwa bado hawajafanya vizuri kiasi cha kutosha katika usimamizi wa ujenzi wa miundimbinu ya huduma za afya licha ya serikali kuwekeza fedha nyingi katika sekta hiyo.
“Kasi ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na ukarabati wa hospitali zetu za wilaya katika mikoa yetu yote 26 ya Tanzania Bara na katika halmashauri zetu zote 184, kwa kweli bado hairidhishi” Alisema Dkt. Dugange.
Aliongeza kuwa “Tuna miradi mingi na ya muda mrefu lakini bado haijakamilika licha ya kwamba imepokea fedha zote kwa mujibu wa BOQ na kwa bahati mbaya baadhi ya miradi haina mipango mikakati ya kuikamilisha, hivyo naomba sote kwa pamoja tufanye tathmini ya ufanisi wa ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa miradi hiyo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Dkt. Dugange amewataka watendaji hao kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao, ili kubaini mapungufu yaliyopo na kuchukua hatua za utatuzi kwa haraka na kwa wakati.
Awali akizungumza katika kikao hicho Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Charles Mahera amesema kikao hicho ni mwanzo wa vikao vya aina hiyo na vingi vitakuwa vikifanyika kwa njia ya mtandao ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wa ngazi za juu katika kuboresha huduma za afya kote nchini.