Imeelezwa kuwa kuongezeka kwa gati jipya katika bandari ya Mtwara kumeongeza mapato yanayokusanywa katika Bandari hiyo kutoka Shilingi bilioni 14 kwa mwaka 2020 na kufikia Shilingi bilioni 23 kwa mwaka 2022.
Akizungumza mara baada ya kutembelea Bandari hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema kukua kwa mapato hayo kumechangiwa na maboresho yaliyofanywa katika bandari hiyo kwa kuongeza gati nyingine kubwa yenye uwezo wa kuhudumia meli yenye uwezo wa kubeba tani takribani elfu 65.
“Serikali imewekeza hapa na ndio maana tunaona matokeo ya kupanda kwa mapato lakini hii isiishie hapa tunahitaji mapato zaidi kwani mzigo wa kupitisha hapa upo wa kutosha ambapo kama tutajipanga vizuri basi tunaweza kukusanya zaidi”, amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete ameeleza umuhimu wa kutangaza zaidi bandari hiyo na kusema kuwa bila kuitangaza bandari hiyo makampuni makubwa kama ya simenti, makaa ya mawe, korosho yanaweza kuendelea kutumia barabara badala ya kutumia bandari.
Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amewataka TPA kuitisha vikao vya mara kwa mara vitakavyowakutanisha wadau wote wa usafiri na usafirishaji ili kujadili namna nzuri ya kutumia bandari hiyo ambayo imeboreshwa kwa kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 150.
Naye Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdilah Salim amemuhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa TPA iko kwenye mpango wa kutenga maeneo kwa wafanyabiashara wakubwa kama Dangote anayesafirisha simenti na Kampuni ya Ruvuma ambayo inasafirisha makaa ya mawe na wasafirishaji wa korosho ili kuhakikisha wanasafirisha mizigo yao kwa wakati bila changamoto zozote.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano, Thomas Mushi amesema tayari juhudi mbalimbali zimeanza kufanyika kwa kuitangaza bandari hiyo ndani na nje ya nchi ili kuwavutia wasafirishaji wengi hususani wa nchi za Zambia na Malawi ambao wanatumia bandari ya Dar es Salaam.
Naibu Waziri Uchukuzi Mwakibete yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku mbili ya kukagua miundombinu inayosimamiwa na taasisi za sekta hiyo.