Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema ujenzi wa Daraja la JP Magufuli lenye urefu wa kilometa 3.2 unaoendelea jijini Mwanza umefikia asilimia 40.2 kazi zinaendelea usiku na mchana.
Mhandisi Kasekenya amezungumza hayo jijini Mwanza, wakati alipokuwa akikagua hatua zilizofikiwa katika mradi huo unaotarajiwa kukamilika tarehe 24 Februari, 2024 na kumuagiza Mkandarasi kuleta vifaa vilivyobakia ili kuongeza kasi ya ujenzi.
“Maendeleo ya ujenzi yanaridhisha na ninakagua mradi mara kwa mara kwa sababu uwekezaji wa hapa ni mkubwa sana ukilinganisha na madaraja mengine yanayojengwa nchini pia teknolojia inayotumika hapa ni ya kipekee hivyo ni jukumu letu sisi kulisimamia kwa karibu”, amesema Mhandisi Kasekenya.
Mhandisi Kasekenya ameeleza kuwa mradi huo ambao unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa shilingi Bilioni 716 ambapo Serikali inaendelea kumlipa Mkandarasi huyo kwa wakati na imedhamiria kukamilisha daraja hili ili wananchi wa jiji hili na mikoa jirani waanze kunufaika na kurahisisha shughuli zao za kiuchumi.
Ameongeza kuwa daraja hilo pindi litakapokamilika litaweza kupunguza muda wa kuvusha watu na magari si zaidi ya dakika nne kulinganisha na hali ya sasa wanapotumia muda mrfu kusubiria kivuko ili kiweze kuwavusha takribani dakika 15.
“Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba inafungua fursa nyingi sana kati ya Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani na baadhi ya nchi tulizopakana nazo ukanda huu”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Aidha, Naibu Waziri Kasekenya, ametoa pole kwa familia ya mfanyakazi aliyepoteza maisha akiwa sehemu ya kazi katika daraja hilo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama eneo la kazi.
Ametoa rai kwa wasimamizi na wafanyakazi wote wanaoshiriki katika mradi huo kuzingatia taratibu na sheria za usalama mahala pa kazi ili kuweza kujilinda wao wenyewe na kuepusha hatari zozote zinazoweza kujitokeza.
“Hii sehemu si salama kwani imezungukwa na maji kila kona hivyo niwaombe wasimamizi kuzingatia usalama wa wafanyakazi wa eneo hili hasa nyakati za usiku na kuhakikisha wafanyakazi wako vizuri kiafya na kuwepo na taa zenye mwanga mkali ili kuepuesha majanga yanayowezajitokeza”, amefafanua Eng. Kasekenya.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza Mhandisi Boniface Mkumbo, ameeleza kuwa mradi huo unaendelea vizuri na mkandarasi ameshaongeza mitambo na wafanyakazi na hadai malipo yoyote kwa kazi zilizokwishafanyika.
Mhandisi Mkumbo, amesema kuwa mradi umeshatoa ajira 801 na kati ya hao wazawa ni 745 sawa na asilimia 93 na wafanyakazi wa kigeni 56 sawa na asilmia 7.
Ujenzi wa Daraja la JP. Magufuli ni sehemu ya mipango ya Serikali ya kulifanya Jiji la Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Maziwa Makuu.