Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujenzi Miundo Werezeshi Mradi wa Umeme Mto Rufiji Wafikia Hatua Nzuri
Nov 21, 2018
Na Msemaji Mkuu

 

Na Veronica Simba – Dodoma

Kazi ya ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kutokana na nguvu za maji ya Mto Rufiji, imefikia hatua nzuri.

Hayo yamebainishwa jana, Novemba 17, 2018 wakati Kamati inayosimamia utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo, ilipokutana na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara jijini Dodoma na kuwasilisha kwake hatua iliyofikiwa.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Juma Iddi alimweleza Waziri Kalemani kuwa kazi ya ujenzi kwa baadhi ya miundombinu wezeshi imekamilika kwa asilimia 100 na baadhi iko katika hatua za mwisho kukamilika.

Mwenyekiti huyo wa Kamati, alitaja baadhi ya kazi zilizokamilika kwa asilimia 100 kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya umeme ya Msamvu- Pangawe na ile inayotoka Dakawa hadi mpakani mwa Pori la Akiba la Selous.

Aidha, nyingine ni ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme vya Pangawe na Dakawa pamoja na kufikisha maji kwenye kambi za ujenzi.

Baada ya kupokea taarifa husika, Waziri Kalemani pamoja na kuipongeza Kamati kwa kazi nzuri, aliitaka kuhakikisha kuwa kazi iliyobaki kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati, ili kumwezesha mkandarasi atakayetekeleza ujenzi wa Mradi huo, kuanza kazi kwa muda uliopangwa.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Hamisi Mwinyimvua, aliitaka Kamati hiyo kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri kwa ufanisi.

Akiitaja miundombinu wezeshi inayojengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huo; Kamishna na Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga alisema ni pamoja na umeme, maji, barabara, reli, viwanja vya ndege, vituo vya afya, mawasiliano na majengo ya makazi na ofisi.

Mradi wa kuzalisha umeme kutokana na nguvu za maji ya Mto Rufiji utakapokamilika, unatarajiwa kuzalisha megawati za umeme 2100.

         

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi