Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uingereza Kusaidia Tanzania Sekta ya Afya
Nov 12, 2024
Uingereza Kusaidia Tanzania Sekta ya Afya
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa kwanza kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John A. Jingu (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Grace E. Magembe (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Kemi Williams (wa kwanza kulia) wakisaini hati za Makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Uingereza ya nyongeza ya pauni milioni 10 (sawa na Tsh bilioni 34), ya kuchangia Mfuko wa Kusaidia ya Sekta ya Afya (Health Basket Fund (HBF) itakaowezesha utoaji wa huduma bora za afya nchini kuanzia mwaka 2024 hadi 2029, iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), jijini Dar es Salaam.
Na Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam.

Tanzania na Uingereza zimesaini hati za makubaliano ya nyongeza ya kuchangia Mfuko wa Kusaidia Sekta ya Afya (Health Basket Fund (HBF)) kati ya Serikali na wadau wa maendeleo (Development Partners) ya pauni milioni 10 (sawa na Tsh bilioni 34), itakayowezesha utoaji wa huduma bora za afya nchini kuanzia mwaka 2024 hadi 2029.

 

Hati hizo zimesainiwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John A. Jingu, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Grace E. Magembe na Mkurugenzi wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Olukemi Williams, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kushoto) na Mkurugenzi wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Kemi Williams, wakibadilishana hati za Makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Uingereza ya nyongeza ya pauni milioni 10 (sawa na Tsh bilioni 34), ya kuchangia Mfuko wa Kusaidia ya Sekta ya Afya (Health Basket Fund (HBF) itakaowezesha utoaji wa huduma bora za afya nchini kuanzia mwaka 2024 hadi 2029, baada ya kusaini Makubaliano hayo katika ukumbi wa ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kusaini hati hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema kuwa Serikali inafuraha kusaini nyongeza ya makubaliano ya awali na sasa Serikali ya Uingereza itatambuliwa kama mmoja wa Washirika wa Maendeleo wanaochangia Mfuko wa Kusaidia Sekta ya Afya kwa mujibu wa makubaliano ya awali (MoU) kati ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo yaliyosainiwa Julai 2021.

 

“Lengo la Mfuko wa kusaidia Sekta ya Afya ni kuunganisha rasilimali za kifedha ili kuboresha huduma za afya nchini Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo mbalimbali ikiwemo Serikali za Jamhuri ya Ireland, Denmark, Uswisi, KOICA, UNFPA na UNICEF, ili kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya kuboresha huduma za afya nchini.

 

Dkt. Mwamba aliongeza kuwa Mchango wa Mfuko wa kusaidia Sekta ya Afya umeleta mabadiliko makubwa katika huduma za afya nchini, kwani imeendelea kupunguza viwango vya vifo vya watoto na kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi za afya katika ngazi ya jamii.

 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, amesema kuwa mfuko wa Afya, tayari umesaidia huduma za afya katika hospitali za wilaya, vijiji, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999.

 

“Tumekubaliana kwa miaka mitano wanatupa pauni milioni 10 (sawa na Tsh bilioni 34) ambazo zitaenda kwenye mfuko wa kusaidia Sekta ya Afya, na tunapoungwa mkono na wadau wetu hawa ni jambo zuri” alisema Dkt. Jingu

 

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Grace E. Magembe, amesema kuwa tangu kuanza ushirikiano na wadau kupitia mfuko kusaidia Sekta ya Afya, Serikali imeongeza kwa idadi kubwa ya vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya ambapo watanzania zaidi ya asilimia 65 hadi 70 wanaweza kupata huduma ndani ya kilomita 5 kutoka wanapoishi.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (Katikati mstari wa mbele), Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John A. Jingu (wa tatu kushoto mstari wa mbele), Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Grace E. Magembe (wa pili kulia mstari wa mbele), Mkurugenzi wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Kemi Williams (wa tatu kushoto mstari wa mbele), Mratibu wa Mfuko wa Afya wa Pamoja kwa Washirika wa Maendeleo, anayemaliza muda wake, Bi. Franziska Freiburghaus (wa kwanza kulia mstari wa mbele) na Kamishna wa Idara Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade ( wapili kushoto mstari wa mbele), wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa Uingereza nchini baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kusaini hati za Makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Uingereza ya nyongeza ya pauni milioni 10 (sawa na Tsh bilioni 34), ya kuchangia Mfuko wa Kusaidia ya Sekta ya Afya (Health Basket Fund (HBF) itakaowezesha utoaji wa huduma bora za afya nchini kuanzia mwaka 2024 hadi 2029, iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), jijini Dar es Salaam.
 

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Kemi Williams, amesema kuwa Serikali ya Uingereza inafahamu umuhimu wa kufikia huduma za afya kwa wote na kuna haja ya kuwa na mifumo ya afya imara na inayoweza kuhimili changamoto kwa njia ya kushirikiana. 

 

“Huduma za afya kwa wote maana yake ni kuwa watu wote, popote walipo au wanapoishi, wanapata huduma bora za afya wanapozihitaji na mahali zinapohitajika bila kuangalia hali zao za kifedha” alisema Bi. Williams

 

Aliongeza kuwa Serikali ya Uingereza inatambua na kupongeza jitihada za kiwango cha juu za Serikali ya Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kufanikisha huduma za afya kwa wote, kama inavyoonekana kupitia mageuzi yanayoendelea katika upanuzi wa huduma za msingi za afya na utekelezaji wa sera ya bima ya afya kwa wote. 

 

“Tunathamini jitihada za kushughulikia mapungufu katika rasilimali watu ili kusaidia kufikia malengo haya na washirika wataendelea kutoa msaada wa kiufundi unaohitajika ili kuboresha ubora wa huduma za afya ya msingi na napenda kuthibitisha tena msaada wa dhati wa Uingereza kwa dira ya Tanzania ya afya kwa wote na kumaliza vifo vinavyoweza kuzuilika ifikapo mwaka 2030” aliongeza Bi. Williams.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi