Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kupambana na rushwa, ufisadi, uzembe na uvivu pamoja na kuimarisha nidhamu kwa viongozi na watendaji wa ngazi zote katika kuwahudumia wananchi.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha wafanyabiashara na wajasiriamali wanaendesha biashara zao kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo pamoja na kujenga tabia ya kuona fahari kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Aprili 4, 2019) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020.
Amesema lengo la Serikali la kuendelea kujenga mazingira mazuri na wezeshi ya kufanya kazi, biashara, kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi ni kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi.
“Ni vema tukatambua kuwa tupo kwenye zama za ushindani wa kiuchumi. Kwa msingi huo, mafanikio yetu katika zama hizi yatategemea pia ubunifu, tija na uwepo wa ufanisi kwenye miundombinu wezeshi ya kiuchumi inayoendelea kujengwa na Serikali.”
Amesema Serikali itaendelea kuonesha uthubutu na dhamira ya dhati katika kukuza uchumi wa viwanda lengo ni kuharakisha ukuaji wa uchumi jumuishi wenye kupunguza umaskini, kuongeza uzalishaji, ajira na ustawi wa watu.
Hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza kwa viongozi, watendaji na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ubunifu na uzalendo katika kujiletea maendeleo.
Kutokana na umuhimu huo, Waziri Mkuu ameielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujenga mahusiano rafiki na walipa kodi badala ya kutumia nguvu na vitisho kudai kodi kwani kwa kufanya hivyo watazorotesha ukusanyaji wa mapato.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli itahakikisha inasimamia ipasavyo rasilimali za Taifa ili zielekezwe katika sekta ambazo zitaliwezesha kufikia malengo pamoja na kuhimili ushindani wa kiuchumi uliopo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kutumia ipasavyo haki yao ya kidemokrasia kwa kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa Oktoba 2019.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha mamlaka zinazosimamia uchaguzi huo, zinashirikiana vyema na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha unaendeshwa kwa amani na usalama.
“Uchaguzi huo ni wa sita tangu kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1994 chini ya mfumo wa vyama vingi vya Siasa. Hivi sasa, Serikali imekamilisha zoezi la uhakiki wa maeneo ya utawala ambayo yatashiriki kwenye uchaguzi huo katika Halmashauri zote 184.”
Waziri Mkuu amesema lengo la uhakiki huo ni kujiridhisha na usahihi wa maeneo hayo kwa idadi na majina ili kufanikisha maandalizi ya bajeti na mahitaji mengine muhimu ya uchaguzi huo ambao maandalizi ya kanuni zake yameshakamilika.
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi katika upigaji kura ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua au kuchaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Oktoba 2019.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu wa 2020, Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na uhakiki wa vituo vya uandikishaji wa wapiga kura.
Amesema uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura nao umekamilika, ambapo kwa upande wa Tanzania Bara vituo vimeongezeka kutoka 36,549 vilivyokuwepo mwaka 2015 hadi kufikia vituo 37,407 mwaka 2018, sawa na ongezeko la vituo 858.
Waziri Mkuu amesema kwa upande wa Zanzibar vimeongezeka vituo 27 kutoka 380 vya mwaka 2015 hadi kufikia vituo 407 mwaka 2018. “Natoa wito kwa wananchi wenye sifa wajitokeze kwa wingi kujiandikisha mara zoezi hilo litakapoanza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L. P. 980,
41193 – Dodoma,
ALHAMISI, APRILI 4, 2019.