Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tunathamini Mchango wa Wadau wa Maendeleo Ukuaji Sekta ya Habari – Mhe. Nape
Jul 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Georgina Misama – MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuinua Sekta ya habari nchini kwa kuboresha mazingira ya Wanahabari na upatikanaji wa taarifa katika mazingira yote sambamba na kusimamia kikamilifu mchakato wa kupitia Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016. 

Akizungumza katika mkutano wa Serikali na Wadau wa maendeleo uliofanyika leo Julai 13, 2022 Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa Wadau wa Maendeleo katika kusaidia ukuaji wa Vyombo vya Habari, upashanaji wa habari na matumizi ya teknolojia nchini.

Aidha, Waziri aliwashukuru Wadau wa Maendeleo kwa jinsi wanavyoshiriki katika  kujadiliana na kubadilishana mawazo na kupanga namna bora ambayo teknolojia inashiriki kusaidia upatikanaji wa habari.

“Uwepo wenu hapa ni ushuhuda tosha wa ushirikiano ulipo baina ya Serikali ya Tanzania na Wadau wa Maendeleo kwani ushirikiano wa Tanzania, UNESCO na Wadau wa Maendeleo ulianza mara tu baada ya Uhuru wa Tanzania mwaka 1961”, alisema Nape

Waziri Nape aliongelea pia suala la mchakato wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambapo alisema ililenga kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya habari ikiwemo ajira, maslahi ya Waandishi wa Habari pamoja na mazingira ya kazi na wajibu katika kutekeleza majukumu yao.

“Serikali imetoa nafasi kwa Wanahabari kuleta maoni mbadala wa yale yanayolalamikiwa na Wanahabari ili kuboresha sheria ya huduma za habari, lengo la mchakato wa maboresho hayo ni kutunga sheria itakayodumu kwa muda mrefu”, aliongeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alizungumzia suala la bodi ya ithibati ambapo alisema ni moja kati ya mambo ambayo yatapitiwa katika mchakato wa Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016.

“Serikali imeonyesha dhamira njema ya kutaka kupitia upya sheria pamoja na taratibu zote ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria hii ya huduma za habari, wadau wameonyesha nia ya kushirikiana na Serikali na waandishi wa habari katika kuhakikisha tunaweka vizuri mazingira katika Sekta hii ya habari,” alisema Msigwa.

Aidha, Msigwa ametoa rai kwa Waandishi wa Habari wote nchini kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zilizopo katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na mchakato wa kupata Sheria ya huduma za habari ambayo itajumuisha maoni ya wadau wote wa habari nchini.

“Kwa mujibu wa utaratibu, sheria inapopitiwa haina maana inazuia sheria iliyopo kufanya kazi, tuonyeshe dhamira njema ya kushiriki kwenye mchakato, tuionyeshe Serikali utayari wetu wa kushikiana. Natumia nafasi hii kuwaomba sana wanahabari na wamiliki wa vyombo vya habari tuzingatie sheria zilizopo,”aliongeza Msigwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi