Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amesema Serikali inapeleka fedha nyingi kwenye Halmashauri zake nchini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, Maji, Barabara na Miradi ya Afya lakini taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo hazifahamiki kwa Watanzania wengi.
Bw. Matinyi aliongea hayo leo Oktoba 29, 2023 wakati alipokutana na Wahariri na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikiwa ni mara yake ya kwanza toka ateuliwe kwenye wadhifa huo.
Kabla ya Mkutano huo, Bw. Matinyi alipata wasaa wa kujitambulisha na kuwafahamisha wadau hao muhimu kwenye Sekta ya habari mipango na mikakati mbalimbali ikiwemo masuala ya Sekta ya habari kwa ujumla.
Amesema Idara ya habari - MAELEZO inatarajia kuzindua programu maalum ya taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo mikoani ifikapo Novemba 1, 2023 mkoani Dodoma, ambapo alisema lengo la programu hiyo ni kuwapa nafasi Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zao kuwaeleza Watanzania nini Serikali imefanya katika maeneo yao.
“Tunataka kuwapa nafasi Wakurugenzi kwa sababu tunataka kusikia habari za utekelezaji wa miradi Katika muundo wa serikali yetu fedha zinapelekwa katika halmashauri na huko ndiko kwenye utekelezaji, tukapozindua program hiyo Dodoma mikoa inayofuata ni Morogoro, Pwani na Dar es Salaam. Kwa awamu hii ya kwanza lakini awamu ya pili tutaenda Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga ” alisema Bw. Matinyi.
Alisema kuna mambo mengi yanaendeshwa kwenye Halmashauri lakini wananchi hawayajui akitolea mfano fedha zinazojulikana kwa jina la ‘asilimia 10 ya Mama’ bado hazifahamiki kwa wengi na kwamba fedha hizo ni asilimia kumi ya mapato ya Halmashauri husika na hutengwa kwa mgawanyo maaalum wa asilimia 4 kina mama, 4 Vijana na 2 kwa watu wenye ulemavu na kuongeza kwamba fedha hizo ni za mkopo unaozunguka na usio na riba.
Vilevile aliongelea masuala ya uelewa wa watanzania katika ufanyaji kazi kwenye Bandari na kusema ipo haja ya kutolewa elimu ili Watanzania waifahamu Bandari ya Dar es Salaam, taasisi zinazofanya kazi kwa kushirikana na bandari pamoja na makusanyo yanayotokana na shughuli zinazoendelea Bandarini hapo.
“Ipo haja Watanzania kufahamu, Bandari ya Dar es Salaam ni kitu gani na kwanini inaibua mijadala mikubwa, tumesikia kwamba asilimia 37 – 40 ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatoka Bandari ya Dar es Salaam na tunatarajia zipande hadi kufikia asilimia 60, je Wanzania wanafahamu fedha hizo ni kodi ya namna gani? Tunataka maswali hayo na mengine mengi Waandishi wa habari muende mkayasikie na kuyaona,”alisema Bw. Matinyi.