Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tunataka Kumuandaa Mtoto Kwenye Safari ya Elimu - Rais Samia
Oct 15, 2023
Tunataka Kumuandaa Mtoto Kwenye Safari ya Elimu - Rais Samia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuashiria ufunguzi wa Shule ya Msingi Imbele, mabweni ya madarasa ya Shule ya Sekondari Mwanamwema Shein kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Manispaa ya Singida Mjini tarehe 15 Oktoba, 2023.
Na Georgina Misama - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi nchini kuhakikisha wanatumia fursa za elimu ambazo Serikali inawekeza kwa ajili ya watoto kuanzia elimu ya Awali mpaka Sekondari.

Aliongea hayo leo Oktoba 15, 2023 wakati akipokea taarifa ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule za elimu ya Awali, Msingi na Sekondari mkoani singida wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo ambapo alisema Serikali imeanza kujenga madarasa kuanzia ya Elimu ya Awali kwa sababu inataka kumuandaa mtoto kwenye safari ya elimu kuanzia akiwa na miaka minne.

“Nimeufungua mradi huu wa elimu kwa niaba ya miradi yote ya namna hii iliyopo nchi nzima, chini ya mradi huu kuna miradi miwili mikubwa ukiwemo wa BOOST unaojenga Shule za Msingi na kuna SEQUIP unaojenga Shule za Sekondari. Shule za aina hii zimejengwa Tanzania nzima, nawaomba wazazi kuhakikisha watoto wanaenda shule kwani hizi ni zetu, naomba tuzilinde ili watoto wengi wafaidike nazo,” alisema Rais Samia.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 230 kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023,  ambazo zilitumwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa Shule za Msingi mpya 302, madarasa ya awali 368, madarasa ya shule za msingi 2,929, nyumba za Walimu 41 (2 in 1) na matundu ya vyoo  2,903.

Alisema hadi Septemba 2023, jumla ya shule mpya 194, madarasa ya awali 294, madarasa ya kawaida 2,303, matundu ya vyoo 2,115 na nyumba za Walimu 23 zimekamilika kujengwa na kwamba miundombinu iliyobaki inatarajiwa kukamilika ifikapo 31/10/2023.

“Katika Mradi wa BOOST, Mkoa wa Singida ulipokea shilingi bilioni 9.02 kwa ajili ya ujenzi wa Shule za Msingi mpya 12, madarasa ya awali 14, madarasa ya msingi 106, nyumba za Walimu 2 na matundu ya vyoo 156, aidha, mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari ni wa miaka 5 kuanzia 2020/2021 hadi mwaka 2024/25 wenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 ambazo zinalenga kujenga shule za sekondari mpya 1,026,” alisema Mhe. Mchengerwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi