Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha Vijana wanapata ujuzi wa kujitegemea kiuchumi, kwa kuanzisha Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kote nchini ili kuwa na Vijana waadilifu, wachapakazi na wazalendo, na hatimaye waweze kuchangia maendeleo katika uchumi wa Taifa.
Amesema mkakati huo unakuja kufuatia kuwepo kwa idadi kubwa ya kundi hilo ambalo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi yake inafikia asilimia 34.5, na hivyo ili kuwaandalia mazingira wezeshi ya ajira, tayari ujenzi wa vyuo hivyo 64 unaendelea katika wilaya kadhaa nchini, huku vingine 50 vikitarajiwa kujengwa.
Ameyasema hayo leo Oktoba 14, 2023 wilayani Babati, Mkoa wa Manyara wakati akihitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa zilizoambatana na kumbukizi ya miaka 24 tangu kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na kilele cha Wiki ya Vijana Kitaifa.
"Ili Uhuru wetu uwe na maana, hatuna budi kudumisha umoja, kwajibika, kufanya kazi kwa bidii na muhimu zaidi kujitegemea, vijana ndio nguzo na nguvu kazi inayotegemewa katika ujenzi wa Taifa lolote lile, na hasa tukidhamiria kujenga Taifa linalojitegemea, nguvu kazi hii ikikosa uelekeo hatutakuwa na msingi mkubwa kwa nchi yetu, na hii ndio mantiki ya kuunganisha Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana Kitaifa",
"Tunataka tujenge nchi yenye vijana waadilifu, wachapakazi na wazalendo ili waweze kuchangia kikamilifu kwenye maendeleo yao wenyewe na Taifa kwa ujumla.” Alimalizia Rais Samia.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bw. Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali yake itaendelea kuiishi falsafa ya Mwenge wa Uhuru ambayo iliasisiwa na Hayati Mwalimu Nyerere kwa ushirikiano na Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shekh Abed Amani Karume ambayo inalenga kudumisha umoja, amani na mshikamano na kuongeza kuwa, Zanzibar itaendelea kuimarisha Muungano na kuwaomba Watanzania kuuheshimu na kuulinda.
Akisoma majumuisho ya risala za utii za Wananchi wa Tanzania kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2023, Bw. Abdallah Shaibu Kaim, amesema kati ya miradi miradi hiyo 1,424 iliyokaguliwa, Miradi saba imebainika kuwa na kasoro kadhaa za utekelezaji na usimamizi, na nyaraka zake zimekabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya uchunguzi.
”Mhe Rais, kwa siku 196, tumefanya kazi ya kuzindua, kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo 1,424 yenye thamani ya shilingi trilioni 5.3, ambayo iligusa sekta za kipaumbele ikiwepo ya elimu, afya, maji safi na salama, barabara, viwanda, kilimo, utawala bora, na uwezeshaji wananchi kiuchumi", alisema kiongozi huyo.
Ameongeza kuwa, katika miradi hiyo, miradi saba yenye thamani ya shilingi bilioni 1.9 imebainika kuwa na kasoro kadhaa ya utekelezaji na usimamizi na hii ni sawa na asilimia 0.5 ya miradi iliyofanyiwa kazi na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu.