Na Mwandishi Wetu - Lushoto
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wameridhishwa na uwekezaji uliofanywa katika kiwanda cha Chai Mponde kilichoko wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.
Wameyasema hayo baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo Kata ya Mponde, Jimbo la Bumbuli Oktoba 15, 2022 ili kuona uwekezaji huo uliofanywa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
“Kwa niaba ya Kamati nichukue fursa hii kuwapongeza, nadhani nyuso zetu mmeziona tumeridhika na kile tulichoona, naomba moyo huu mliyoanza nayo msiipunguze muendelee nayo.”Alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. George Malima ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mpwapwa.
Alisema kazi ya Kamati yake ni kuangalia pale ambapo Serikali imeweka mitaji.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameruhusu fedha nyingi kuja kwenye kiwanda hiki ili muweze kuwekeza na hivyo kutoa ajira za kutosha na kuinua maisha ya Watanzania, hiyo ndiyo hasa nia ya Mheshimiwa Rais.” Alibainisha.
Naye Dkt. Julius Chaya ambaye ni Mbunge wa Manyoni na Mjumbe wa Kamati hiyo ya PIC alisema wakati wawekezaji hao walipokutana na Kamati hiyo jijini Dodoma, waliona wazo hilo la uwekezaji ni zuri sana kwani uwekezaji ndio umeweza kukuza ajira kwenye maeneo mbalimbali duniani.
“Tunawapongeza mnapofufua hivi viwanda, wananchi wanapata ajira, wakulima nao wanapata mahala pa kuuza mazao yao, kwa kweli tunaishukuru Serikali lakini pia tunaishukuru Mifuko yote kwa kazi nzuri.” Alisisitiza Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar na Mjumbe wa Kamati, Mhe. Mariam Mwinyi.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe wametoa ushauri kuwa ni lazima uongozi wa kiwanda uhakikishe wamejipanga vizuri katika eneo la masoko hususan yale ya nje, kwani wanunuzi wakubwa wa bidhaa za kilimo licha ya kusisitiza ubora lakini pia hupenda hakikisho la kupata bidhaa kwa mwaka mzima bila kusitisha.
Akiwakaribisha kiwandani hapo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Emmanuel Humba alisema wamefarijika sana na ujio wa Kamati kwani ni ishara ya kutambua juhudi zilizofanywa na wawekezaji hao watatu.
“Kiwanda hiki kama mlivyoona kinawahusu wananchi, wawekezaji tunaongeza nguvu tu, lakini watakaofanya kiwanda hiki kifanye kazi ipasavyo ni wananchi wenyewe.” Alisema.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema, kusudio kubwa la kukifufua kiwanda ni kuwawezesha wananchi wa Lushoto, Bumbuli Korogwe na maeneo jirani kupata kipato na hivyo kuwainua kiuchumi kwani wengi wanategemea zao hilo.
“Tunategemea kwamba kiwanda kitanufaisha takriban asilimia 70 ya wakulima wa chai kutoka Lushoto, Bumbuli Korogwe na maeneo jirani," alifafanua Dkt. Mduma.
Akizungumzia hatua za utekelezaji wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya kiwanda hicho, Bw. Anselim Peter alisema awamu ya kwanza ya kufufua kiwanda hicho ilikuwa ni kukarabati majengo na mitambo ambayo ilikufa kabisa, wakati awamu ya pili ilikuwa ni kuboresha kiwanda kwa ujumla wake na kutengeneza menejimenti.
“Karibu asilimia 100 kiwanda kimekamilika, tumeshaanza mchakato wa kuajiri wafanyakazi ili kusudi tunapoanza uzalishaji kamili tuweze kutekeleza majukumu ya kiwanda ipasavyo.” Alisema.