Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameeleza kuwa, Serikali imeamua kutekeleza mradi wa umeme wa maji ya Rumakali (MW 222) wenye thamani ya Shilingi trilioni 1.4 uliopo wilayani Makete mkoani Njombe ili kuwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha kutoka vyanzo mbalimbali vya nishati.
Alisema hayo tarehe 29.07.2022 akiwa katika Kijiji cha Rumaga wilayani Makete baada ya kutembelea eneo ambalo mradi utatekelezwa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili mkoani Njombe ambapo pamoja na kukagua miradi ya nishati, alisikiliza kero za wananchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Makamba alisema kuwa katika Bajeti ya mwaka 2022/2023, Shilingi bilioni 8 zimetengwa kwa ajili ya kazi za maandalizi ambazo zinajumuisha masuala mbalimbali kama vile utayarishaji wa nyaraza za zabuni, uthaminishaji na ujenzi wa miundombinu wezeshi ikiwemo barabara.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo aliwaahidi kuwa, kila mwananchi atakayepisha mradi atalipwa fidia stahiki na ametoa wito kwa wananchi hao kujiandaa na fursa mbalimbali zitakazotokana na mradi huo ikiwemo ajira na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo za chakula, malazi na usafiri.
Ili mradi huo wa maji na mingine iweze kuwa endelevu, Waziri Makamba alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji na kwamba Wizara ya Nishati kupitia TANESCO imetenga fedha za kutosha Kwa ajili ya kushiriki kwenye shughuli za uhifadhi wa mazingira.
Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga aliishukuru Serikali kwa kutenga fedha hizo za kuanza kutekeleza mradi huo wa Rumakali na kueleza kuwa wananchi wameshaanza kuchangamkia fursa za kuhudumia watu takriban 7000 watakaokuwa kwenye mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda alisema kuwa mradi huo ukianza utakuza ajira wilayani humo na kuongeza mzunguko wa fedha hivyo alimuahidi Waziri wa Nishati kuwa Wilaya hiyo itashirikiana na Wizara ya Nishati kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Kuhusu hali ya umeme wilayani humo, alisema kuwa inaridhisha na upatikanaji wa mafuta pia unaridhisha.
Kuhusu usambazaji umeme vijijini alisema kuwa, Wilaya hiyo ina vijiji 93 ambapo ni vijiji 37 tu ambavyo bado havina umeme na kwamba mkandarasi anaendelea na kazi na fedha kiasi cha Shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.