Tume ya Utumishi wa Walimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) wameendesha mafunzo ya kuwaaandaa wataalamu ngazi ya taifa wa kutoa mafunzo ya Mfumo wa Tathmini na Upimaji wa Wazi wa Utendaji Kazi (OPRAS) kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na sekondari nchini.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku nne mfululizo na kuhitimishwa mwishoni mwa wiki jijini Dodoma yamewandaa wawezeshaji ngazi ya Taifa ambao watakwenda kuwajengea uwezo wawezeshaji katika ngazi ya Malaka za Serikali za Mitaa.
Wawezeshaji ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa wanatarajiwa kutoa mafunzo kwa Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu ambao nao watatoa elimu hiyo kwa waalimu wanaowasimamia katika shughuli za kila siku na ambao ndio walengwa wakubwa wa mafunzo hayo.
Akitoa mada katika Mafunzo hayo, mmoja wa Maafisa wanaoshughulikia masuala ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Neema Lemunge alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali katika matumizi ya OPRAS kwa walimu kitu kinachopunguza ufanisi katika kufikia malengo ya kazi.
“Mwezi Februari, 2017 Serikali kwa kushirikiana na Mradi wa PS3 ilifanya utafiti kubaini sababu zinazofanya OPRAS kuendelea kuwa changamoto kwa watumishi wa umma na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo” alisema.
Alitaja changamoto zilizobainishwa kuwa ni kutokuwepo kwa uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa OPRAS kwa walimu, kutokuwepo kwa usimamizi thabiti katika kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kama inavyotakiwa pamoja kutokuwepo kwa taratibu madhubuti katika kufanya ufwatiliaji na tathmini.
Aliongeza kuwa “changamoto nyingine iliyobainishwa ni suala la ujazaji wa fomu ya OPRAS hususan katika kuweka sahihi wa malengo ya mtumishi unaoshabihiana na upimaji sahihi wa utendaji wa kazi”.
Alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali kwa nyakati mbalimbali imechukua hatua za kurejesha uthabiti wa matumizi ya mfumo huo zikiwemo kufanya tafiti pamoja na kutoa nyaraka za maelekezo na miongozo ya kutekeleza mfumo huo.
Ameeleza kuwa Serikali iliweka mikakati ya namna ya kulifanyia kazi suala la kujaza fomu ya OPRAS ikiwemo kuzitambua kada za utumishi wa umma zenye uhitaji mkubwa wa ufumbuzi katika uwekaji malengo, kuchambua mwongozo unaoelekeza namna ya uwekaji malengo na kupendekeza utaratibu wa uwekaji malengo na kutoa elimu kwa watumishi wa ngazi hizo ili utaratibu pendekezwa uanze kutumika.
Naye mmoja wa wakufunzi katika mafunzo hayo kutoka PS3, Bw. Geofrey Lufumbi alisema kuwa lengo la mradi wa PS3 ambao unafanya kazi katika Mikoa 13 yenye Halmashauri 93 ni kutoa msaada wa kitaalamu kwa Serikali katika kuimarisha mifumo ya sekta za umma ili kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma kwa jamii.
Hivyo, mafunzo hayo yatasaidia kuongeza tija kwa walimu ambapo watakuwa wanajiwekea malengo mahusus, yanayopimika, yanayofikika, yenye uhalisia na ambayo yanawekewa muda maalum wa utekelezaji.
Mafunzo hayo yaliwahusisha Walimu, Maafisa Utumishi na Maafisa Elimu kutoka Halmashauri mbalimbali, Kaimu Katibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kutoka Wilaya mbalimbali, maafisa kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu Makao Makuu, TAMISEMI pamoja na Maafisa wa Mradi wa PS3.