Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tume ya Madini Yapokea Ripoti Ukaguzi Migodi ya Madini ya Vito, Kinywe
Jun 29, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Samwel Mtuwa - Dodoma

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya leo tarehe 28 Juni, 2018,amepokea ripoti ya Ukaguzi Maalum wa Migodi ya Madini ya Vito na Madini ya Kinywe (Graphite) kutoka kwa Mwenyekiti wa Timu ya Ukaguzi Profesa Justinian Ikingura.

Ripoti hiyo imetokana na Tume Maalum ya Wataalam Sita iliyoundwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof. Manya tarehe 17 Juni, 2018 ikilenga kufanya ukaguzi maalum katika maeneo ya uchimbaji wa madini ya Vito na Kinywe katika wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro.

Aidha, ukaguzi huo ulilenga kutekeleza maelekezo ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko aliyoyatoa hivi karibuni wakati wa ziara yake mkoani Morogoro.

Katika ziara ya Naibu Waziri Biteko mkoani humo,alipokea malalamiko kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini ya vito ambao ni wanakijiji wa kijiji cha Epanko kilichopo katika eneo la mradi wa madini hayo.

Aidha, kufuatia malalamiko hayo Naibu Waziri aliahidi kuunda timu ya watalaam wa madini itakayofanya kazi ya ukaguzi maalum kwa lengo la kutathmin uendeshwaji wa migodi ya madini ya vito na kinywe pamoja na biashara ya madini kulingana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake.

Katika ripoti hiyo,timu ya wataalam wa madini imetoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo Serikali kupitia Wizara ya Madini na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuweka mkakati wa kufanya Utafiti na tathmin ya madini adimu ya vito katika eneo la Mahenge na maeneo mengine nchini ili kuwepo na takwimu sahihi za kuvutia wawekezaji katika uchimbaji wa madini hayo.

Pendekezo lingine ni Mamlaka husika kuweka mpango wa kutoa huduma ya uthaminishaji wa madini ya vito katika maeneo ya wachimbaji wadogo ili kuwezesha wachimbaji hao kupata bei stahiki ya madini wanayozalisha na hivyo kuongeza kipato chao na kulipa tozo stahiki kwa Serikali.

Wajumbe wa timu hiyo walitoka katika Taasisi ya Jiolojia ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Chuo cha Madini Dodoma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Ukaguzi wa Migodi naAfisa Madini Mkazi wa Dodoma.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi