Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tukiwatumikia Watu, Tunamtumikia Mungu-Rais Dkt. Samia
Aug 15, 2023
Tukiwatumikia Watu, Tunamtumikia Mungu-Rais Dkt. Samia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta utepe pamoja na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dkt. Dickson Chilongani kuashiria ufunguzi rasmi wa Jengo la Kitega Uchumi (Safina House) la Kanisa hilo kwenye sherehe zilizofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Jijini Dodoma tarehe 15 Agosti, 2023. Engine katika picha ni Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Mhashamu, Dkt. Maimbo Mndolwa pamoja na Maaskofu wengine wa Kanisa hilo nchini.
Na Paschal Dotto-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amelitaka Kanisa la Anglikana pamoja na taasisi nyingine za kidini kuwafundisha vijana maadili mema pamoja na bidii ya kufanya kazi ili kujiletea maendeleo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo la kitega uchumi (Safina House), leo Agosti, 15, 2023 Jijini Dodoma, Rais Samia amesema kuwa kanisa linatakiwa kuwatumikia watu na ndiyo dhana kamili ya kumtukia Mungu.

“Nataka nitoe wito kwa Kanisa Anglikana kuwa muwafundishe vijana lakini si vijana tu hata wakubwa ambao wanalitumia kanisa vibaya kufanya mambo ya hovyo naomba kemeaneni ili kuweka maadili mema, pamoja na  kazi kubwa iliyofanyika lakini nataka kuhimiza kazi ya kulinda maadili ya jamii na  kumtumikia Mungu kunaanza na kuwatumikia watu, Tukiwatumikia watu, tunamtumikia Mungu,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema kuwa Kanisa Anglikana ni taasisi ambayo imekuwa ikishirikiana na Serikali katika kutoa huduma za kijamii ikiwemo Elimu kupitia shule na vyuo na kwenye sekta ya kilimo Pamoja na sekta zingine za uzalishaji.

Dkt. Samia, alisema kuwa kufanya kazi kwa pamoja kati ya Serikali na Sekta za kidini ikiwemo Kanisa Anglikana ni kuongeza kasi ya maendeleo ya taifa na kulifikisha pale linatakiwa kufika lakini litafika kwa kufanya kazi pamoja.

“Hapa nataka nitoe wito kwa Kanisa Anglikana hususani Dayosisi hii ya Central Tanganyika kuendelea kuwahubiria waumini wenu kuhusu kufanya kazi kwa bidii na kuchangamkia fursa mbalimbali zitokanazo na Serikali kuhamia Dodoma tunataka maendeleo ya Dayosisi hii yaendane na maendeleo ya Jiji la Dodoma”, Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amelipongeza kanisa Angelikana kwa jengo hilo ambalo litapamba Jiji la Dodoma na kuongeza uchumi wa Dayosisi ya Central Tanganyika na amesema kuwa Serikali itaendelea kutambua mchango wa kanisa Angelikana na itaendelea kudumisha ushirikiano na kanisa hilo.

Kwa Upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dkt.Maimbo Mndolwa, alisema kuwa kanisa Anglikana linafanya kazi mbalimbali ukiachana na kazi za injili pia linatoa huduma za Elimu, Afya na kwenye sekta ya kilimo,

“Kanisa halifanyi kazi za injili pekee bali linafanya na kazi za maendeleo na za kijamii, hayo yote tunayafanya tukijua ya kwamba mkono wa Mungu unagusa watu kwa njia nyingi na moja ya sababu ya kufanya haya ni kugusa maisha ya watu wenye uhitaji mkubwa”, Alisema Dkt. Mndolwa.

Dkt. Mndolwa alisema kuwa Dayosisi  ya Central  Tanganyika  inajishughulisha  na huduma za elimu, afya na jamii ikiwemo hospitali, shule za sekondari, chuo kikuu cha St. John na Chuo cha Ualimu kilichopo Muleba, Kagera kwa kazi ya kutoa elimu iliyobora kwa wananchi.

Dayosisi ina shule 9, kati yake mbili ni za msingi (english medium), shule mbili za sekondari na shule moja ya kimataifa inayotumia mtaala wa cambridge, tumeanzisha shule ya ufundi ya viziwi kwa kutumia lugha ya alama, shule ya msingi ya wasioona, wenye uono hafifu na walemavu wa ngozi.

Aidha, alieleza kuwa kwa kipindi cha takriban miaka 10, Dayosisi imeweza kusomesha watoto yatima takriban 7,000 kwa ngazi ya shule ya msingi, sekondari, elimu ya ufundi na vyuo vikuu kwa kuwapatia lishe bora, vifaa na sare za shule, kuwalipia ada na matibabu.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi