Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TSC Yatakiwa Kufanyia Kazi Hoja Zilizowasilishwa Kwenye Maonesho ya Nanenane
Aug 09, 2023
TSC Yatakiwa Kufanyia Kazi Hoja Zilizowasilishwa Kwenye Maonesho ya Nanenane
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Angellah Jasmine Kairuki akiongea na watumishi wa OR – TAMISEMI na Taasisi zake walioshiriki kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa na Kimataifa yaliyofanyika mkoani Mbeya.
Na Mwandishi wetu – Mbeya.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Angellah Jasmine Kairuki ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuzifanyia kazi hoja zote zilizowasilishwa na wateja ambao wengi wao ni Walimu wakati wa maonesho ya wakulima Nanenane ili kuendelea kuondoa changamoto za Walimu nchini.

 

Waziri Kairuki ametoa agizo hilo alipotembelea banda la TAMISEMI na Taasisi zake tarehe 8 Agosti, 2023 katika kilele cha maeonesho ya Nanenane Kitaifa na Kimataifa yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Angellah Jasmine Kairuki akisaini Kitabu cha wageni tarehe 8 Agosti, 2023 alipotembelea banda la Ofisi ya Rais TAMISEMI na Taasisi zake kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa na Kimataifa yaliyofanyika mkoani Mbeya.

 

 “Natambua kuwa mmepokea hoja nyingi za wateja waliotembelea kwenye banda lenu na wateja wengi ni Walimu. Hoja zilizotolewa siyo za Walimu wa Mkoa wa Mbeya peke yake ukienda maeneo yote utakuta ni hizohizo. Nendeni mkazichambue na kuzipatia ufumbuzi ili Walimu wetu waendelee kutekeleza majukumu yao kwa amani na Utulivu,” amesema Waziri Kairuki.

 

Akisisitiza agizo hilo, Waziri Kairuki amesema miongoni mwa kero kubwa ambazo TSC inapaswa kuzifanyia kazi ni Walimu kucheleweshwa kupandishwa vyeo, kupandishwa madaraja bila kuzingatia utaratibu kitu kinachosababisha kutofautiana kwa vyeo kwa Walimu wa kundi rika moja, Walimu wanaopanda vyeo pamoja kuidhinishiwa barua za kupanda vyeo kwa tarehe tofauti kwa sababu za kimfumo na kucheleweshwa kubadilishiwa cheo baada ya kujiendeleza kielimu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (wa tatu kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa OR – TAMISEMI na Taasisi zake walioshiriki kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa na Kimataifa yaliyofanyika mkoani Mbeya. 

 

Pamoja na hayo, Waziri Kairuki amewataka watumishi wote wa OR – TAMISEMI na taasisi zake kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na moyo wa kujituma ili kuendelea kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza malengo yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.

 

“Ninajua watumishi wa OR - TAMISEMI pamoja na Taasisi zetu mna uwezo mzuri wa kufanya kazi na mnatekeleza majukumu yenu vizuri. Kama tunavyojua Ofisi ya Rais TAMISEMI ndiyo inayohudumia wananchi moja kwa moja, na sisi watendaji ndio tunaotegemewa katika utoaji wa huduma hizo. Hivyo, kila mmoja wetu ahakikishe anatimiza wajibu wake ipasavyo ili Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan aweze kufikia malengo yake katika kuwaletea maendeleo wananchi,” amesema Waziri Kairuki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi