Kongamano la Chama cha Wanataaluma wa Sayansi ya Uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) lililokuwa likifanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 26 mwaka huu limefikia tamati jana (28.10.2022) ambapo baada ya majadiliano ya kina yaliyokuwa yakihusu tafiti mbalimbali zilizolenga kuboresha sekta za Mifugo na Uvuvi, wataalam hao wamefikia maazimio kuhusu tafiti hizo.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Dkt. Jonas Kizima amesema kuwa wanataaluma hao kwa pamoja wamebaini kuwa ni lazima zifanyike tafiti za kutafuta vyakula mbadala na vyenye ubora vya Mifugo na samaki ili viwasaidie wadau wanaojishughulisha na shughuli za ufugaji kuzalisha zaidi.
“Lakini tumeona athari za mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri sana uzalishaji wa mifugo kwa hiyo tumekubaliana ni lazima zifanyike tafiti ambazo zitaibua aina ya malisho na mifugo inayoweza kukabiliana na mabadiliko hayo”, ameongeza Dkt. Kizima.
Dkt. Kizima amebainisha jambo jingine walilobaini kupitia kongamano la wataalam hao kwa mwaka huu kuwa ni umuhimu wa bima ya mifugo ambapo wamejadili kwa kina umuhimu wa bima hiyo na kuainisha manufaa mbalimbali ambayo mfugaji anaweza kupata kupitia bima hiyo.
“Kingine ambacho kimefanyika kupitia kongamano la mwaka huu ni wasilisho la namna ambavyo taratibu za kitafiti zinapaswa kupata kibali cha maadili yanayohusu utafiti huo, hivyo kuanzia sasa kabla hujachapisha tafiti zako kwenye majarida ya mitandaoni ni lazima uwe na kibali hicho kitakachoonesha ni kwa kiasi gani umezingatia maadili ya taaluma hiyo”, Amesema Dkt. Kizima.
Awali akizungumza katika hotuba yake ya kufunga kongamano hilo aliyoisoma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Bw. David Lyamongi amesema kuwa mkoa huo kwa sasa unatekeleza maazimio ya wanataaluma hao kwa vitendo kupitia elimu ya namna ya kuboresha shughuli za ufugaji inayotolewa na Vyuo vya Nelson Mandela, Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kituo cha Tengeru na Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC).
“Mkoa wetu ni moja ya mikoa inayofanya shughuli za ufugaji kwa kiasi kikubwa na tayari tumeshaanza kufuga kisasa kwa kupunguza idadi ya mifugo na kuiboresha michache inayobaki ili kumuongezea tija mfugaji mwenyewe na Taifa kwa ujumla,” Amesema Bw. Lyamongi.
Akizungumzia kuhusu kuongeza idadi ya washiriki kwenye Kongamano lijalo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Zabron Nziku ametoa wito kwa wataalam wa sekta za Mifugo na Uvuvi waliopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kushiriki kwenye kongamano hilo ili waweze kuongeza ujuzi utakaowawezesha kwenda kuwahudumia vizuri wananchi kwenye maeneo yao.
“Lakini pia nitoe rai kwa wadau wa sekta binafsi wanaojishughulisha na sekta za Mifugo na Uvuvi, kushiriki kwa wingi na kuja kutoa elimu juu ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha ili wawatumie wataalam wanaoshiriki kongamano hili kama mabalozi wa bidhaa zao pindi watakapoenda kule chini kwa watumiaji wa bidhaa hizo.” Amehitimisha Dkt. Nziku.
Mbali na majadiliano ya kina kuhusu tafiti za Mifugo na Uvuvi, Kongamano hilo la Chama cha wanataaluma wa sayansi ya uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) kwa mwaka huu liliambatana na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanataaluma wa chama hicho kwenda kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha utalii wa ndani nan je kupitia filamu yake ya “Royal Tour”.