Shilingi Trilioni 3.7 kutumika katika ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 2,035 .
Ujenzi wa barabara hizo umebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Agosti 26 ,2023 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
" Wakandarasi wa kutekeleza miradi hii tayari wamepatikana na mikataba ya ujenzi wake imeshasainiwa ili kazi iendelee", alisisitiza Msigwa.
Akitaja miradi hiyo Msigwa amesema wa kwanza ni ule wa Kidatu , Ifakara, Lupiro Malinyi , Kilosa, Mpepo, Londo, Lumecha hadi Songea wenye urefu wa kilomita 512.
Mradi mwingine ni ule wa Arusha, Kibaya hadi Kongwa wenye urefu wa Kilomita 493.
Msigwa aliongeza kuwa mradi mwingine ni wa Handeni, Kibereshi, Kijingu, Njoro, Olboroti, Mrijo chini, Dalai, Bicha, Chambolo, Chemba, Kwa Mtoro Singida wenye urefu wa Kilomita 460.
Miradi mingine ni pamoja na ule wa Igawa, Songwe hadi Tunduma wenye urefu wa kilomita 218.
Pia, mradi wa Masasi Nachingwea wenye urefu wa Kilomita 81.
Mradi wa mwisho kwa mujibu wa Msigwa ni ule wa Karatu, Mbulu, Hydom, Sibiti, Lalago hadi Maswa mkoani Shinyanga wenye urefu wa Kilomita 389.
Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo katikati ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege na mingine kwa lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi.