[caption id="attachment_33566" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya makusanyo ya kodi ya Mwaka wa Fedha 2017/18 ambayo yameongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 15.5 kutoka shilingi trilioni 14.4 kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 sawa na ongezekeo la asilimia 7.5.[/caption]
Na Veronica Kazimoto
Makusanyo ya kodi kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 yameongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 15.5 kutoka shilingi trilioni 14.4 kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 sawa na ongezekeo la asilimia 7.5.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya makusanyo ya kodi ya mwaka wa fedha 2017/18, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo amesema kuwa katika mwezi Juni, 2018 pekee, TRA imekusanya jumla ya shilingi trilioni 1.5 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.4 kwa mwezi Juni, 2017 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 8.0.
“TRA inapenda kuwapongeza na kuwashukuru walipakodi wote ambao mchango wao umeiwezesha Serikali kupata mapato haya tunayotangaza leo kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na za jamii zikiwemo ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara, ununuzi wa ndege, upatikanaji wa elimu, afya na mambo mengine kwa manufaa ya watanzania wote,” alisema Kayombo.
Kayombo amezitaja sababu zilizosababisha kuongezeka kwa makusanyo hayo kuwa ni pamoja na elimu ya kodi kuzidi kueleweka kwa walipakodi na wananchi kwa ujumla, kuongeza ukaribu na walipakodi kwa kuwasikiliza na kutatua changamoto zao za kikodi, kuongezeka kwa walipakodi wapya kupitia kampeni ya kuwasajili kwa kuwafuata waliko na kurahisisha ulipaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisema kuwa, katika Mwaka huu wa Fedha 2018/19, TRA imedhamiria kutekeleza kwa vitendo kampeni kabambe ya msamaha wa riba na adhabu kwa malimbikizo ya madeni ya nyuma na inategemea kuongeza urahisi wa kulipa madeni ambayo yalikuwa kikwazo kwa wafanya biashara wengi kulipa na hata kuendelea na biashara.
“Vilevile, mamlaka imedhamiria kuongeza kasi ya usajili wa walipakodi wapya. Hivyo, tunaendelea na kasi ya utambuzi na usajili wa wafanyabiashara wadogo ili kila mtu anayestahili kulipa kodi asajiliwe na kuchangia kikamilifu maendeleo ya Taifa,” alieleza Kayombo.
Mkurugenzi Kayombo ametoa wito kwa walipakodi na wananchi wote kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kujenga utamaduni wa kudai Risiti za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kila mfanyabiashara anapofanya mauzo na mnunuzi anatakiwa kudai risiti kila anaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.