Na.Prisca Libaga - Arusha.
MAMLAKA ya mapato, nchini TRA, mkoani Arusha imelazimika kuifungia kampuni ya utalii ya Tanzania Game Tracker (TGT) kutokana kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi kwa kipindi kirefu.
Akizungumza Ofisini kwake Jijini Arusha Leo Meneja wa TRA, Mkoa wa Arusha, Faustine Mdessa amesema kwamba Ofisi yake imefikia hatua hiyo kutokana na wamiliki wa kampuni hiyo kutokuwa tayari kulipa sehemu ya deni licha ya kuwepo mkataba unaowataka walipe kidogokidogo ili kumaliza deni hilo.
Amesema kabla ya kuifungia kwa makufuli kampuni hiyo TRA ilifanya utafiti na kubaini kuwa inadaiwa deni kubwa linalotokana na malimbikizo na hivyo kutoa maamuzi ya mwisho ya kuifungia kampuni hiyo ambayo imeshindwa kutoa ushirikiano kwa TRA.
Meneja huyo wa TRA alisema, mara walipobaini kuwa kampuni hiyo ilikuwa inadaiwa kodi kubwa ambayo isingeliweza kulipwa yote kwa mkupuo mmoja,waliingia makubaliano kati ya TRA na kampuni hiyo iwe inalipa kwa awamu malimbikizo hayo lakini kampuni hiyo imeshindwa kutekeleza makubaliano hivyo TRA imeamua kuifungia.
Amesema kuwa TRA,ipo kwenye ukusanyaji wa kodi ya kila mwezi na sasa inaendesha operesheni kwa wafanyabiashara mbalimbali ambao wanadaiwa kodi ili waweze kulipa na kufanya biashara bila ya usumbufu.
Amesema kuwa TRA ina makundi ya aina mbili za wafanyabiashara kundi moja ni lile lisilotaka usumbufu ni la walipaji wazuri wa kodi lakini kuna kundi lingine ni wakaidi,wakorofi ,wajeuri hivyo inalazimika kutumia njia mbalimbali ili kuhakikisha wanapatikana na kulipa kodi wanayodaiwa.
Bw. Mdessa, ameongeza kuwa TRA, haihitaji kutumia nguvu wala haipo kwa ajili ya kuwakomoa wafanyabiashara bali inataka wafanyabiashara wote kuwa waungwana kwa kulipa kodi zao kwa wakati na hivyo kuepuka usumbufu na kutozwa faini kwa kuchelewa.
Aidha TRA, imekuwa ikitoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati kuwasilisha taarifa zao TRA, pindi zinapohitajika na hata wafanyabiashara kufika TRA kwa majadiliano zaidi pindi kunapotokea matatizo katika ulipaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya TGT,Michael Allard alikiri kwamba ni kweli kampuni hiyo imefungiwa na TRA na wamepata mshtuko kutokana na kufungiwa kampuni yao ambapo maafisa wa TRA walifika juzi jioni na kufunga kufuli kubwa ambalo limeathiri utendaji.
Amesema suala hilo la wao kulipa kodi lipo mahakamani sababu wao wanajua hesabuni zao na TRA nayo inahesabu yao hivyo wapo tayari kukaa na TRA ili ofisi hiyo ifunguliwe.
Allard amesema wamefungiwa na TRA kwa sababu kampuni yao haijalipa kodi na wapo tayari kukaa meza moja na TRA ili kumaliza mzozo huo wa kodi sanjari na kuitoa kesi mahakamani.