Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TPB Kulipa Fidia kwa Wateja Benki ‘Mufilisi’
Dec 13, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Waandishi Wetu, Dodoma

BENKI ya Posta Tanzania (TPB) imepewa jukumu la kulipa fidia kwa waliokuwa wateja wa benki tano zilizofungiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Richard Malisa aliyasema hayo jana alipokuwa akiwasilisha mada ya Bodi ya Bima ya Amana na Ufilisi wa Mabenki na Taasisi za fedha: Mafanikio na Changamoto, wakati wa warsha ya waandishi wa habari za uchumi na biashara jijini Dodoma.

Alisema TPB imepewa jukumu hilo tangu mwezi Oktoba mwaka huu, ikiwa ni hatua ya kurahisisha ulipwaji wa fidia hizo zinazotolewa na Bodi ya Bima ya Amana , ambapo benki hiyo ina matawi mengi nchini yatakayorahisisha kuwafikia walengwa.

Kwa muujibu wa Malisa, benki zilizofungiwa mwaka huu ni tano, ambazo ni  Meru Community Bank,  Njombe Community Bank,  Kagera Farmers’ Cooperative Bank,  Efatha Bank Limited pamoja na Covenant Bank for women Tanzania Ltd.

Malisa alisema mpaka mwezi Oktoba mwaka huu, DIB imelipa fidia kwa wateja wa benki hizo kuanzia kati ya Shilingi 20,000 hadi milioni moja na laki tano kwa asilimia 97%.

“Kwa mujibu wa sheria na taratibu za DIB tunatoa fidia ya kiasi chote au sehemu ya amana ya mteja aliyokuwa ameweka kwenye benki husika" alisema.

Aidha alisema bodi hiyo mpaka kufikia Aprili 31, mwaka huu imekuwa na jumla ya shilingi bilioni 357.5 ikiwa ni michango kutoka kwa benki zipatazo 53 ambazo huwajibika kisheria kuchangia Mfuko wa Bima ya Amana.

Malisa alisema kufungwa kwa benki tano kwa pamoja kumesababisha bodi kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wafanyakazi, muda mrefu wa uhakiki wa taarifa za wateja kufuatia kukosekana taarifa kamili kama vile picha au namba za mawasiliano za mteja.

“Kukosekana kwa uelewa, na wateja kutojitokeza kwenye malipo ya fidia, hizi ni baadhi ya changamoto tulizokabiliana nazo,” alisema Malisa.

Kutokana kadhia iliyojitokeza kwenye ulipaji wa fidia hizo, mtaalam huyo aliwashauri wananchi kuwa makini kabla na baada ya kufungua akaunti ya benki.

“Usiweke fedha kwenye benki ambayo huna uhakika nayo, kwa kufanya hivyo utasaidia kulinda mfuko ili uwe na uwezo wa kuhudumia wananchi (wateja), lakini pia usalama wa fedha zako.” Alisisitiza.

Alisema, kwa mujibu wa sheria ya BoT, Benki inapoanzishwa lazima iwe na mtaji wa kima cha chini cha shilingi bilioni 15, na benki hiyo haishauriwi kumkopesha mtu mmoja familia au kampuni moja asilimia 20 ya mtaji wake.

Bodi ya Mfuko wa Bima ya Amana huwajibika kutoa fidia kwa wateja wa benki iliyofungwa au kufa kwa kutoa fidia isiyozidi shilingi milioni 1.5, huku mteja aliyeweka amana chini ya kiasi hicho cha fedha atapata fedha zake zote.

Mwisho

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi