Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Timu Zote za Taifa Zifanye Maandalizi ya Kutosha katika Mashindano ya Kimataifa
Sep 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Eleuteri Mangi-WUSM

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Mhe. Aloyce Kamamba amesema timu zote za taifa zifanye maandalizi ya kutosha ili kuwakilisha vema taifa katika mashindano ya kimataifa.

Mhe. Kamamba amesema hayo Septemba 2, 2022 baada ya kupokea na kujadili taarifa iliyowasilishwa na Wizara hiyo kwenye kamati hiyo kuhusu utendaji wa taasisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

“Sisi kama kamati tumesisitiza Wizara kwamba timu zote za taifa ziwe za wanawake, wanaume ama walemavu zipate muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi, isiwe muda mfupi. Ipate muda wa maandalizi wa kutosha pamoja na fedha ili kile cha muhimu katika timu hiyo kama imeandaliwa vizuri kiweze kupatikana kwa timu kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali”, amesema Mhe. Kamamba.

Timu hizo za taifa zinasimamiwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ni muhimu kwa taifa katika kusimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini.

Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema siri kubwa ya mafanikio ya Wizara hiyo ni ushirikiano mkubwa kati ya Viongozi wa Wizara na watumishi wote kuhakikisha malengo ya kuwatumikia watanzania katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo yanafikiwa.

Ili kuhakikisha vipaji vya Sanaa na Michezo kwa vijana vinaendelezwa, Naibu Waziri Mhe. Gekul amesema wanafunzi wanaofanya vizuri katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA wataendelezwa kupitia shule maalum za michezo 56 ambazo ni mahususi kwa kuendeleza vipaji vya Sanaa na Michezo.

Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesema kuwa Wizara imetenga Shilingi bilioni 2 kuhakikisha shule 56 za kulea vipaji vya wanamichezo zinakuwa na miundombinu ya michezo ambayo itasaidia kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali nchini na kuongeza kuwa Wizara hiyo imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 10 kuhakikisha kunakuwa na viwanja saba vyenye ubora unaotakiwa kimataifa kwa michezo mbalimbali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi