Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Thamani ya Mfuko wa Pensheni Kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Yafikia Trilioni 5.8
May 31, 2019
Na Msemaji Mkuu

 

Na Frank  Mvungi

Thamani ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imefikia Trilioni 5.8 hali inayoonesha kuwa mfuko huo unaendelea kuimarika na hivyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama wake.

Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo  Bw. Hosea  Kashimba  amesema kuwa  kuunganishwa kwa mifuko ya GEPF, LAPF, PSPF na PPF kunatoa  fursa ya kuimarisha zaidi sekta ya hifadhi ya Jamii hali iliyochangia thamani ya mfuko mpya wa PSSSF kuendelea kukua hata katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake.

“Tumeshatumia zaidi ya Trilioni moja kulipa mafao kwa wanachama wetu hali inayoonesha kuwa mfuko upo katika hali nzuri hivyo niwatoe hofu wanachama wetu kwani tumejipanga kuhakikisha tunawahudumia vizuri kwa mujibu wa sheria na kanuni za hifadhi ya jamii “ Alisisitiza Kashimba

Akifafanua Kashimba amesema kuwa,  wastaafu elfu kumi wameshalipwa mafao yao tangu kuanzishwa kwa mfuko huo na wachache ambao hawajalipwa ni wale ambao hawajahakiki taarifa zao kwa muda  uliotolewa hivyo aliwata kujitokeza na kuhakikiwa ili warejeshwe katika daftari la malipo. “Ukishahakikiwa tunakurejesha kwenye daftari la malipo na utalipwa malipo yako yote ambayo hukuwa umelipwa hapo awali kabla ya kuhakikiwa hivyo niwatoe hofu wanachama wetu na kuwataka wajitokeze kuhakiki taarifa zao” Alisisitiza Kashimba

Alieleza kuwa,takribani wastaafu 113,000 wamehakikiwa kati ya wastaafu 124,000 waliotakiwa  kuhakikiwa hivyo kuwaomba wanachama wa mfuko huo nchini kuendelea kujitokeza kuhakikiwa kupitia ofisi  za mikoani kwa kuwa huduma zinazotolewa makao makuu  zinatolewa pia mikoani.

Akizungumza kuhusu ujenzi wa uchumi wa viwanda Bw. Kashimba amesema kuwa mfuko huo umejipanga kikamilifu kuendelea kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza  katika sekta mbalimbali kulingana na miongozo ya Serikali.

“Tumewekeza katika Kiwanda cha viatu Karanga Moshi kwa ubia na Jeshi la Magereza na tunatarajia Kiwanda hiki kitatoa ajira  elfu nne na kuzalisha jozi milioni 1. 2 kwa mwaka, tunawekeza kwenye kiwanda cha kuchakata tangawizi kichopo Wilayani Same, Kiwanda cha nyama Morogoro na vingine kulingana na miongozo ya uwekezaji na maagizo ya Serikali “Alisisitiza Kashimba

Aidha, Mitambo ya kuzalisha viatu katika  Kiwanda  Karanga inatarajiwa kuwasilisi nchini na kufungwa katika kiwanda hicho kabla ya mwisho wa mwaka huu ili kutekeleza azma ya sekta hiyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi jumuishi kupitia viwanda.

Hata hivyo Kashimba aliwataka wanachama wote kuhakikisha kuwa waajiri wanawasilisha michango yao kwa wakati ili kuepuka usumbufu wakati wa kustaafu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa mfuko huo Bw. Victor Kikoti amesema kuwa baadhi ya mafao yanayotolewa ni yale ya muda mfupi na muda mrefu lengo likiwa kuwawezesha wanachama wote kuishi maisha bora hata baada ya kustaafu.

“Wanachama wetu wataendelea kunufaika na huduma zetu na hata pale inapotokea bahati mbaya mwanachama wetu amefariki basi haki zake hazitapotea na zinalindwa kwa mujibu wa sheria ili ziwanufaishe warithi wake” Alisisitiza Kikoti

Naye Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Bw. Gilbert Chale amesema kuwa mfuko huo umejenga mifumo bora inayounganisha Ofisi zote na makao makuu ya mfuko ili kuimarisha huduma na tija kwa wanachama.

Kuunganishwa kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF, GEPF, LAPF na PSPF kumewezesha kuanza rasmi kwa mfuko mpya wa Hifadhi ya Jamii katika Utumishi wa Umma (PSSSF) mwaka 2018.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi