Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TFS Yaanza Kumtua Mama Ndoo kichwani - Naibu Waziri Masanja
Aug 26, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeanza kumtua mama ndoo kichwani kwa vitendo kwa kujenga mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi milioni 22 katika kijiji cha Butengo Kata ya Butengorumasa Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa katika hafla fupi ya uzinduzi wa mradi katika kijiji cha Butengo.

“Mwaka huu kauli mbiu ni kumtua mama ndoo kichwani, hivyo TFS tumeanza kuwatua kinamama ndoo kichwani na tunawatua kwa sababu wamekuwa na mchango mzuri kwenye hifadhi hii” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amewataka viongozi wa Kata na Vijiji kusimamia vizuri mradi huo ili ulete manufaa yaliyokusudiwa ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji.

“Serikali za vijiji, kata muwe makini katika kusimamia mradi huu kwa kuwa hii ni rasilimali yenu na mkiiharibu ni nyie wenyewe lakini tunatamani muitunze ili tunapoleta miradi mingine tuone faida za miradi hiyo” Mhe. Masanja ameongeza.

Aidha, amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Butengo kwa jitihada kubwa wanazozifanya za kulinda Shamba la Miti Silayo, kwa kutunza maeneo ya hifadhi na kuwa na mahusiano mazuri na wahifadhi.

Mhe. Masanja ametoa rai kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi nchi nzima kuiga mfano wa wananchi wa Kijiji cha Butengo ambao kwa hiari yao wamekubali kushirikiana na wahifadhi.

”Ninyi mmekuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi na sisi kama Serikali lazima tutimize yale mtakayoyaomba” amesema.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Dkt. Merdad Kalemani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka miradi 11 ya maji katika Jimbo la Chato ukiwemo mradi uliofadhiliwa na TFS.

Amesema uwepo wa mradi huo utapunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Butengo.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu Shamba la Miti Silayo, Juma Mwita amesema mradi huo uliogharimu kiasi cha Shilingi milioni 22.1 unahudumia vitongoji vitatu vya Butengo Senta, Butengo na Mwenge ambapo jumla ya Kaya 180 sawa na wastani wa watu 1,080 wananufaika.

Mradi huu umekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwa kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji kwani muda mwingi ulikuwa ukitumika kutafuta maji na umewezesha upatikanaji wa maji safi na salama.

Pia, amesema mradi huo umewezesha kupungua kwa magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama kama kichocho, kuhara na kipindupindu.

Mradi wa maji wa Butengo ulianzwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi