[caption id="attachment_30728" align="aligncenter" width="900"] Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) , Dkt. Kassimu A.Nihuka akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya dhana ya Elimu ya Sekondari nje ya mfumo rasmi, kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Karibu Tanzania Organization (KTO) Bw.Maggid Mjengwa.[/caption]
Na Mwandishi wetu
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeandaa mafunzo ya siku tano ili kuwajengea uwezo walimu 30 kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na TEWW Jijini Dar es Salaam, Programu hii ijulikanayo kama “ Elimu Haina Mwisho- Skills Development Program For Young Women Through Folk Development Colleges ” inalenga kukuza kiwango cha elimu hapa nchini.
Sehemu ya taarifa hiyo imeeleza kuwa programu hiyo imegawanyika katika awamu mbili na inalenga Wanawake na Vijana ambao wamekatishwa masomo kwasababu mbalimbali ikiwamo mimba za utotoni.
“ Mafunzo haya yanaandaliwa na Karibu Tanzania Organization (KTO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) pamoja na Taasisi ya Aflatoun International ya Uholanzi na Wakfu wa Mastercard(Mastercard Foundation) “ Imesisitiza sehemu ya taarifa hiyo.
Mafunzo yanayotolewa ni ya miaka miwili ikiwamo elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi, ujasiriamali, stadi za maisha na ufundi.
[caption id="attachment_30731" align="aligncenter" width="900"] Mkurugenzi wa Karibu Tanzania Organization (KTO), Bw. Maggid Mjengwa (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu majukumu ya KTO na maeneo ya ushirikiano na TEWW. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa bodi ya KTO Bw. Aidan Mchawa na kulia Kaimu Mkurugenzi wa TEWW Dkt. Kassimu A. Nihuka.[/caption]Jukumu hili linaendana na jukumu la kisheria la TEWW la kuandaa na kutoa mafunzo kwa walimu, wawezeshaji na wasimamizi wa elimu ya watu wazima nchini. Washiriki wa mafunzo haya ni wakufunzi wa vyuo vitatu vya maendeleo ya wananchi (FDC) nchini kutoka Mbinga FDC (Ruvuma), Bigwa FDC (Morogoro) na Masasi FDC (Mtwara).
Pia taarifa hiyo imebainisha kuwa Watakapomaliza mafunzo hayo, wakufunzi hao waliojengewa uwezo watarudi kufundisha kwenye vyuo vyao, Programu ni ya miaka minne na inalenga kuvifikia vyuo vyote 55. Wanawake Vijana 10,000 watanufaika na program hii.
TEWW ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Namba 12 yamwaka 1975 na kupewa majukumu mbalimbali. Pamoja na majukumu mengine, Taasisi inajukumu la kutoa elimu ya sekondari kwanjia ya Ujifunzaji Huria na Masafa (UHM) pamoja na kuandaa wataalamu wa elimu ya watu wazima na Maendeleo ya Jamii .
Asasi ya KTO inayofanya kazi pamoja na vyuo vyote 55 vya Maendeleo ya Wananchi kwenye kutekeleza programu mbalimbali kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi.
Programu hii yenye kuwalenga Wanawake Vijana itakuwa njia mbadala ya kuwasaidia walengwa kwenye kusonga mbele kwenye maisha na kuchangia kwenye kuinua uchumi wa Taifa ilikuifikisha Tanzania ya viwanda, hivyo TEWW na KTO imeandaa mafunzo kwa waalimu wa vyuo vya maendeleo ya Wananchi ili kuwajengea uwezo wa namna ya kuendesha programu hii.
[caption id="attachment_30732" align="aligncenter" width="900"] Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu toka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Bi. Happiness J. Magoma akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) mchango wa Wizara hiyo katika miradi ya KTO. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TEWW Dkt. Kassimu A. Nihuka.[/caption]Aidha kwa kushirikiana na KTO Kaimu Mkurugenzi wa TEWW Dkt. Kassimu Nihuka amefafanua kuwa, TEWW kupitia programu hii inatoa fursa kwa wanawake vijana waliokatisha elimu yao kwasababu mbalimbali ikiwamo ndoa za utotoni, kukimbia ukeketaji na hata kukatishwa masomo yao kwa ujauzito kupata elimu mbadala.
Elimu hiyo itatolewa katika maeneo ya ufundi,stadi za maisha, stadi za fedha, ujasiriamali na elimu ya Sekondari. Utolewaji wa mafunzo hayo itasaidia kupanua soko la ajira ikiwamo uwezo wa kuajiriwa, kujiajiri na kupata sifa ya kuendelea zaidi na masomo.
Hivyo, programu hii inawalenga Wanawake Vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ili wapate fursa ya kupata elimu ya mafunzo ya ufundi, ujasiriamali na elimu ya Sekondari. Kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Karibu Tanzania Organization wamekusudia kwa dhati kuboresha maisha ya wanawake vijana waliokosa fursa katika mfumo rasmi ili waweze kujiajiri au kuajiriwa hivyo kuboresha maisha yao na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
Aidha, Mkurugenzi wa KTO alisema kuwa programu hii imeshirikisha Shirika lisilo la kiserikali la Uholanzi la Aflatoun International na Mfuko wa wakfu wa Kimataifa wa Mastercard (Mastercard Foundation)
KTO kwa kushirikiana na TEWW inawakaribisha wote kujiunga na programu hii itakayotekelezwa kwa kuanzia kwenye Vyuo Vya Maendeleo ya wananchi vya Mbinga, Masasi na Bigwa kwa mwaka 2018. Mkurugenziwa KTO, Bw. Maggid Mjengwa ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati wa kufunga mafunzo kwa Wakufunzi wa Vyuo vya MaendeleoyaWananchi.
Karibu Tanzania Organization (KTO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) pamoja na Taasisi ya Aflatoun International ya Uholanzi na Wakfu wa Mastercard(Mastercard Foundation) imeandaa mafunzo ya siku tano ili kuwajengea uwezo walimu 30 kutoka Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi. Programu hii ijulikanayo kama – Elimu Haina Mwisho- Skills Development Program For Young Women Through Folk Development Colleges.
,