Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TET, Ukombozi Watia Saini Mkataba Uendelezaji Urithi wa Ukombozi Barani Afrika
Aug 11, 2023
TET, Ukombozi Watia Saini Mkataba Uendelezaji Urithi wa Ukombozi Barani Afrika
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana wakishuhudia utiaji saini hati ya makubaliano ya uendelezaji historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika. Makubaliano hayo yamesainiwa leo Agosti 11, 2023 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth Komba na Mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Bw. Boniface Kadili.
Na Grace Semfuko, MAELEZO.

 

Taasisi ya elimu Tanzania (TET) na Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika wametia saini hati ya makubaliano ya uendelezaji historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika ambapo watashirikiana katika kuandaa maudhui ya historia ya ukombozi na kuingizwa kwenye vitabu vya kiada na ziada.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyofanyika leo Agosti 11, 2023, imeshuhudiwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt Pindi Chana ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana kutoa mafunzo kwa Walimu waliopo kazini na Walimu tarajali waliopo vyuoni ambayo yatawawezesha kutumia njia mbalimbali katika kufundishia.

Akizungumza mara baada ya makubaliano hayo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema ni muhimu Tanzania ikahifadhi historia ya ukombozi wa Bara la Afrika, ili vizazi vijavyo vitambue namna ambavyo Viongozi wa Nchi ya Tanzania walivyopambania uhuru wao na wa Mataifa mengine ya Bara la Afrika.

“Tusipojua tulipotoka, hatutajua tunapoenda na historia ya urithi wetu itapotea, njia ya kwanza ya kujua sisi kama watanzania, kama wana Bara la Afrika lazima turudi nyuma tujue tulipotoka, harakati za ukombozi ni muhimu, kumbukumbu ambazo zinatunzwa hapa ni muhimu kwa Bara la Afrika na ni muhimu kwa vizazi vyetu, ni muhimu kujua kuwa Tanzania iliongoza harakati za ukombozi ni muhimu watu wetu wajue, kulikuwa na ubaguzi wa rangi na elimu.”  amesema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda amesema ni muhimu vitabu vya urithi wa ukombnozi vichapishwe kwa wingi na kusambazwa katika mashule na maktaba mbalimbali ili watanzania na watu wa Afrika wajue thamani ya ukombozi wa nchi zao.

Kwa upande wake Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema makubaliano hayo yamekuja wakati muafaka kwani Wizara yake na Wizara ya Elimu walishaanza mazungumzo kuhusu kuingizwa kwa program za historia ya urithi wa ukombozi katika mitaala hiyo ikiwa na  lengo kuelezea Tanzania ilifanya nini katika kusaidia nchi nyingine kupata uhuru.

“Utiaji Saini uliofanyika hapa tulishajadiliana sana wakati wa Bunge, sisi tulishaanza mazungumzo kwamba katika mitaala yetu tutaweka program za urithi wa ukombozi, hata kwenye michezo tukasema tutaweka mitaala hii ya urithi wa ukombozi ili watu wote wajue Tanzania ilifanya nini katika kusaidia nchi zingine, kwa hiyo historia ni lazima kuitunza katika maktaba zetu, janga linalotutafuna ni kutokuelewa historia yetu, lazima tuwe na maadili, lazima tuwe na taifa lenye utamaduni unaoeleweka, lugha yetu ya kiswahili, muarobaini wake ni hii leo ni lazima tuwe na vitabu vinavyoonesha historia yetu ya Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika” amesema Balozi Dkt. Chana.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema makubaliano hayo yanahusu kuhifadhi urithi wa ukombozi kwenye kuandaa vitabu vinavyoelezea kumbukumbku ya ukombozi wa Bara la Afrika na kuingizwa kwenye mitaala ya kaunzia darasa la nne pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu yatakayowezesha wanafunzi kujua historia ili kuwa na kizazi cha wanafunzi ambao ni weledi katika kutunza na kuenzi, na kujivunia historia ya Bara la Afrika.

“Tumekubaliana kushirikiana katika kuandaa, kuhuisha maeneo mbalimbali ya maeneo ya uhuishaji wa ukombozi wa Bara la Afrika, maudhui ya historia ya ukombozi wa Bara la Afrika yameanza kuingizwa kuanzia vitabu vya darasa la nne ambayo  yanahusisha katika kuandaa vitabu vya kiada na ziada, tutajitahidi kuhakikisha kunakuwa na vitabu vya ziada vya kutosha na tutawahamasisha wachapaji waje kuchukua maudhui ya kutosha” amesema Dkt. Komba.

Katika hafla hiyo, Mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Ukombozi wa Bara la Afrika Bw. Boniface Kadili amesema kituo hicho kina maudhui ya kutosha kuwawezesha wanafunzi kufahamu kwa ukubwa mchango wa Tanzania kwa mataifa ya Bara la Afrika ya kupata uhuru wao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi