Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) inatarajia kutekeleza vipaumbele tisa ikiwa ni muendelezo wa kutekeleza majukumu ya Udhibti na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika pamoja na Uhamasishaji wa maendeleo ya Sekta ya Ushirika nchini.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Benson Ndiege ameeleza vipaumbele hivyo leo jijini Mbeya wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mwelekeo wa bajeti ya taasisi hiyo mwaka huu wa fedha.
“Vipaumbele tulivyojiwekea kwa mwaka huu ni pamoja na kuratibu uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ili kuchochea maendeleo ya Ushirika nchini, kufanya uthamini wa mali zinazomilikiwa na Vyama vya Ushirika kwa lengo la kutambua thamani halisi ya soko ya mali hizo na hivyo kuviwezesha vyama kufanya uwekezaji wenye tija na kuanzisha Mfuko wa Bima ya Akiba na Amana za SACCOS utakaotumika kama kinga ya akiba na amana za wanachama wa SACCOS ambao SACCOS zao zitashindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria”, alisema Mrajis wa Vyama hivyo.
Alitaja vipaumbele vingine vikiwemo vya kuimarisha udhibiti na usimamizi wa Vyama vya Ushirika kwa kutoa mafunzo kwa maafisa Ushirika 226, kuanza matumizi ya Mfumo wa Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika, kuhamasisha, kuratibu na kusimamia ujenzi na ufufuaji wa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao, kuratibu na kuhamasisha ujenzi wa maghala ya mazao ya kilimo, kutengeneza utaratibu wa uwezeshwaji vyama vya ushirika na kuimarisha zaidi matumizi ya Vyombo vya Habari.
Dkt. Ndiege amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kutumia mfumo wa ushirika katika kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuchangia ipasavyo katika ustawi wao na wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, katika kutekeleza hilo ameongeza kuwa, kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha Ushirika unahamasishwa miongoni mwa Watanzania na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha Wanaushirika.
Kutokana na utekelezaji unaoendelea kila mwaka, taasisi hiyo imeongeza uwekezaji katika Vyama vya Ushirika ambao umesababisha ongezeko la ajira kutoka 100,100 mwaka 2020/2021 hadi 146,555 mwaka 2021/2022 na kati ya ajira zilizopatikana, za kudumu ni 31,819, za mkataba ni 28,