Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TCDC Kuzindua Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika
Aug 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO


Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), inatarajia kuzindua Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika mwishoni mwa mwezi  huu wa Agosti, 2022.


Hayo yamebainishwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Benson Ndiege wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Mbeya kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya taasisi hiyo kwa mwaka 2021/22 na mwelekeo wa bajeti kwa mwaka 2022/23.


Dkt. Ndiege amesema kuwa, Tume katika mwaka 2021/2022, ilijiwekea vipaumbele vya utekelezaji hususan katika maeneo ya kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika, kuratibu uhamasishaji, utafiti na utoaji wa elimu ya maendeleo ya Ushirika, kuimarisha masoko, uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi.


“Katika upande wa kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika, Tume iliamua kuandaa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika mfumo utakaomrahisishia mkulima na mwanaushirika kupata taarifa sahihi za utendaji katika Ushirika”, alisema Dkt. Ndiege.


Amefafanua kuwa, mfumo huo utaangalia maeneo ya uwekezaji, mikopo ya pembejeo, marejesho ya mikopo kwa mkulima, bei  pamoja na malipo ya mazao ya mkulima. 


Ameongeza kuwa, taarifa za Mfumo huo zitaweza kupatikana pia kupitia simu ya mkononi. 


Sekta ndogo ya Ushirika ni Sekta wezeshi inayojumuisha Vyama vya Ushirika vya aina mbalimbali vilivyoko katika Sekta mbalimbali  ikiwemo, Kilimo, Fedha, Madini, Mifugo, Viwanda na Usafirishaji. Sekta hii inasimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) ambayo ni Idara ya Serikali inayojitegemea iliyo chini ya Wizara ya Kilimo.


Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi