Serikali imepokea fedha za msaada wa Dola Milioni Moja zilizotolewa na Serikali ya China kupitia Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kusimamia na kudhibiti usafiri wa anga na hivyo kuchochea ongezeko la mashirika ya ndege kutua na kuruka hapa nchini.
Fedha hizo ambazo ni matokeo ya ukaguzi mbalimbali ambao umekuwa ukifanywa na ICAO kwa nchi zote zinazotoa huduma za usafiri wa anga ili kuhakikisha kuna usalama wakati wote ambapo Tanzania ni miongoni mwa wanufaika.
Akizungumza katika hafla maalum ya uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema fedha hizo zitatumika kuboresha miundombinu ambayo kwa sasa inafanyika sambamba na maboresho yanayofanywa na Serikali katika Shirika la Ndege Nchini.
“Nawapongeza sana Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kwa kazi nzuri ambayo mmeifanya mpaka kuwa miongoni mwa nchi chache ambazo zimepata fedha hizo, ni imani yangu kuwa hatutarudi nyuma hasa ukizingatia Serikali inaboresha Shirika letu la Ndege”, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Naibu Waziri huyo ameitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha fedha zinasimamiwa vizuri ili kuleta tija na matokeo shahiki ili kubaki kwenye viwango vya juu vya usimamizi na udhibiti wa usafiri wa anga nchini.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Anga Duniani, Kanda ya Mashariki na Kati (Estern and Southern African), Bw. Barry Kashambo, amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCAA jitihada mbalimbalimbali ambazo amekuwa akizifanya ambapo ndani ya miaka miwili ameipandisha asilimia za usalama na udhibiti kutoka asilimia 50 na kufikia asilimia 67 na kufanikiwa kupata mkopo kutoka katika Shirika hilo.
Kwa upande wake Mshauri wa Waziri kutoka Ubalozi wa China, Bw. Xu Chen, amesema Serikali ya China itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya Taifa.
Awali akitoa taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Hamza Johari, amesema fedha hizo zitaekelezwa kwenye mafunzo ya wataalam katika eneo la Usalama na ununuzi wa vifaa mbalimbali ili kuimarisha udhibiti na kuongeza usalama katika usafiri huo.